WANATAALUMA NA WAHITIMU UDOM WAKUTANA KUJADILI ATHARI CHANYA ZA AI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, December 16, 2025

WANATAALUMA NA WAHITIMU UDOM WAKUTANA KUJADILI ATHARI CHANYA ZA AI


 Na Mwandishi Wetu- Dodoma 

Wanataaluma na wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), leo Desemba 16,2025 wamekutana jijini Dodoma katika Kongamano la 16 la kitaaluma kukijadili kwa kina athari chanya za matumizi ya teknolojia, hususani akili Unde (Artificial Intelligence – AI), katika kukuza elimu, utafiti na maendeleo ya jamii.

Kongamano hilo, lililowakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali za elimu na teknolojia limeelezwa kuwa jukwaa muhimu la kubadilishana maarifa na uzoefu kuhusu namna teknolojia ya kisasa inavyoweza kutumika kama chombo cha kuboresha utoaji wa huduma, kuongeza tija katika kazi na kuibua fursa mpya za ajira kwa vijana.

Akizungumza mara baada ya kongamano hilo, Makamu Mkuu wa chuo hicho Prof. Lughano Kusiluka amesema akili Unde ni aina ya teknolojia ambayo haikwepeki, hivyo katika ulimwengu wa sasa ambao teknolojia za kidijitali zinakwenda kwa kasi wanataka iwe na athari chanya.

"Kwakweli katika eneo hilo vijana wetu wanafanya vizuri, na katika taasisi ambazo katika nchi hii kwasasa unaweza kuzungumzia wanao toa vijana wazuri kwenye masuala ya teknolojia za kidigitali nafikiri UDOM iko juu sana,"amesema. 

Mbali na hayo Profesa Kusiluka amesema matamanio yao ni kuona watanzania hawawi nje ya wakati huu ambao teknolojia kama akili Unde inatumika ulimwenguni kote, hivyo wanadhani ni jambo la msingi kwa kuwa sehemu nyingi imesaidia kuleta maendeleo kwa kasi.

Aidha, amefafanua juu ya aina ya mitihani wanayoitoa kwa watahiniwa kutokana na namna ambavyo akili Unde inaendelea kushika hatamu ulimwenguni, amesema wanatamani wasimtahini Akili Unde bali mwanadamu aliyekuja kusoma chuoni hapo.

"Kwahiyo hata aina ya mitihani tunayoitoa inazingatia kuwa zipo teknolojia ambazo zikitumika vibaya zinaweza zisizalishe vijana ambao ni wazuri, kwahiyo ipo aina mbalimbali ya kufanya mitihani ikiwemo ile ya vitendo lakini hapa Akili Unde haitakuwa inazungumza kwa niaba yao,"amefafanua. 

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo maalum ya Kiuchumi (TISEZA), Gilead Teri amesema chuo Kikuu UDOM kimeendelea kuwa nguzo ya uongozi ya kuzalisha viongozi, wajasiriamali, wafanyabiashara na watumishi ambao wanakuwa na mchango mkubwa kwenye Taifa. 

"Amesema kwasasa akili mtambuka inahitajika sio kuishia tu kwenye elimu lazima kujifunza na mambo mengine ya ziada pamoja na kuangalia masuala mazima ya teknolojia katika kazi zetu zote tunazo zifanya, hivyo tukiweza kuunganisha hivi vyote viwili tunapata matokeo makubwa zaidi, "amesema. 

Kwa upande wao, wahitimu wa UDOM walioshiriki kongamano hilo wamesema litakuwa na tija kuwa na chachu zaidi ya kwenda kukabilkana na ukuaji wa teknolojia. 

Kongamano la 16 la wanataaluma na wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dodoma limehitimishwa kwa wito kwa taasisi za elimu ya juu nchini kuwekeza zaidi katika teknolojia za kisasa, hususani akili unde, ili kuandaa rasilimali watu yenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya dunia ya sasa na ya baadaye.









No comments:

Post a Comment