Na WMJJWM - Morogoro
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Wizara za kisekta pamoja na Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) imeanza zoezi la kufanya tathmini ya utendajii kazi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) kwa kipindi cha miaka mitano 2020/2021 - 2024/2025.
Lengo la zoezi hili ni kutathmini mchango wa NGOs katika utekelezaji wa miradi na afua mbalimbali, uzingatiaji wa sheria na kanuni zinazosimamia NGOs, utekelezaji wa Mwongozo wa Uratibu wa NGOs Tanzania Bara na Mkakati wa Kitaifa wa Uendelevu wa NGOs, pamoja na utekelezaji wa majukumu ya Bodi ya Uratibu wa NGOs na Baraza la Taifa la NGOs.
Timu ya Wataalam kutoka Wizarani iliyoongozwa na Afisa Ufuatiliaji na Tathmini Mkuu wa Idara ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Charles Komba imeanza kazi hiyo Disemba 1 - 3, 2025 mkoani Morogoro kwa kufanya uchambuzi wa nyaraka mbalimbali ambazo zimetoa picha halisi ya mafanikio, changamoto, fursa na matarajio ya Mashirika hayo katika kuongeza ufanisi na utambuzi wa mchango wao katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Komba amesema wanafanya tathmini hiyo ili kujua kwa kina mchango wa Mashirika hayo katika Maendeleo ya Taifa, ambapo pamoja na zoezi hilo wamepata nafasi ya kusikia ushuhuda kutoka kwa wanufaika wa huduma mbalimbali zinazotolewa na Mashirika hayo hususani katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.
"Tumefanikiwa kutembelea miradi na kuzungumza na wananchi walionufaika na huduma zinazotolewa na mashirika manne: Kinara For Youth Evolution inayotoa mafunzo ya ushonaji kwa wasichana, taulo za kike kwa wanafunzi na mtandao wa elimu ya kujikinga na vihatarishi vya mimba za utotoni na vijana kujiepusha na makundi hatarishi; Shirika la Education Gauge for Growth Tanzania linayojihusisha na huduma ya uchimbaji wa visima vya maji, huduma ya vitabu kwa shule mbalimbali na usarifi kwa wanafunzi; Shirika la PELUM Tanzania ambalo linahusika na kutoa elimu ya kilimo na uwezeshaji kiuchumi; na Shirika la Agriwezesha Tanzania linalotoa elimu ya ufugaji wa samaki na kuku, utunzaji wa mazingira kupitia upandaji wa miti, uzalishaji wa mafuta ya alizeti pamoja na kilimo cha uyoga". amesema Komba.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Taifa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Morogoro, Otanamusu Nicholaus ambaye pia ameshiriki zoezi hilo, ametoa rai kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutoa ushirikiano na taarifa sahihi za utekelezaji pamoja na changamoto wanazopitia ili Serikali iyafanyie kazi na kuyapatia ufumbuzi.
Kwa upande wake mmoja wa mnufaika wa huduma ya maji inayotolewa na Shirika la Education Gauge for Growth Tanzania, Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mbuyuni, Rose Mwakibinda amesema huduma ya hiyo ya Maji imekuwa na manufaa makubwa kwa shule kwa kuwezesha kuwa na maji safi na salama, kufanya usafi wa mazingira ya shule ili kuepuka magonjwa ya mlipuko.









No comments:
Post a Comment