Na OWM – TAMISEMI, Mwanza
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amesema Serikali kupitia Mradi wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) imetumia kiasi cha Shilingi Bilioni 67 kujenga Barabara na Masoko ili kuwahudumia wananchi wa Mwanza.
Prof. Shemdoe ametoa taarifa hiyo leo Januari 24, 2026 Jijini Mwanza, wakati alipopewa nafasi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba ya kuzungumza na wananchi wa mwanza waliojitokeza kumsikiliza mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo na kuzindua meli ya New MV Mwanza.
Prof. Shemdoe amefafanua kuwa, fedha hizo zinatumika kujenga barabara ya Nyamaghana yenye urefu wa kilomita 14 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 22, barabara ya Ilemela yenye urefu wa kilomita 12 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 24, soko la samaki Mkuyuni Nyamaghana lenye thamani ya Shilingi Bilioni 7 pamoja na soko la mazao mchanganyiko Ilemela lenye thamani ya Shilingi Bilioni 14.
Akizungumzia hatua ya ujenzi wa barabara hizo, Prof. Shemdoe amesema zimekamilika na ziko kwenye hatua ya kuweka taa za barabarani ili wananchi waweze kuzitumia nyakati za usiku huku wakiwa salama.
“Mhe. Waziri Mkuu ikikupendeza pindi barabara zikikamilika, tutakuomba uje kuzizindua rasmi kwa ajili ya kuanza kutumiwa na wananchi wa Mwanza na watanzania wote watakaokuja Jijini Mwanza kwa shughuli mbalimbali,” Prof. Shemdoe amewasilisha ombi.
Mhe. Prof. Shemdoe amemhakikishia Waziri Mkuu kuwa, ofisi yake itaisimamia vema TARURA ili miradi yote ya barabara, soko la samaki na soko la mazao mchanganyiko ikamilike kwa wakati, na hatimaye wanachi waanze kunufaika na uwepo wa miradi hiyo.






No comments:
Post a Comment