Baraza la Michezo la Taifa (BMT) leo tarehe 20 Januari, 2026, limekutana na wadau wa michezo kutoka sekta mbalimbali katika mkutano maalum wa kukusanya maoni kuhusu marekebisho ya Sheria za Baraza la Michezo la Taifa. Mkutano huo umefanyika katika Ukumbi wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Lengo kuu la mkutano huo lilikuwa ni kukusanya maoni, mapendekezo na ushauri kutoka kwa wadau wa sekta ya michezo, yatakayosaidia kuboresha utendaji wa Baraza la Michezo la Taifa pamoja na kuimarisha misingi ya maendeleo ya michezo nchini. Aidha, mkutano huo ulilenga kuweka mazingira bora ya kisheria yatakayochochea ukuaji wa sekta ya michezo kwa kuzingatia mabadiliko ya wakati na mahitaji ya sasa.
Marekebisho yanayopendekezwa yanakusudia kuipa michezo tafsiri pana zaidi, ikiwemo kuitambua michezo kama chanzo cha kipato, biashara na nyenzo muhimu ya kukuza utalii wa michezo nchini. Hatua hii inalenga kuhakikisha sheria zinaboreshwa ili ziendane na dira ya maendeleo ya sekta ya michezo na fursa zake za kiuchumi.
Aidha, maoni na mapendekezo yatakayokusanywa yatawasilishwa katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kabla ya kufikishwa Bungeni kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa.
Kwa ujumla, marekebisho hayo yanalenga kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika usimamizi wa sekta ya michezo, pamoja na kuweka mazingira rafiki yatakayochochea maendeleo endelevu ya michezo kwa maslahi mapana ya Taifa.
Katika mkutano huo, Baraza la Michezo la Taifa liliwakilishwa na Afisa Sheria wa BMT, Bw. Thadeus Almas, pamoja na Msajili wa Vyama vya Michezo Tanzania, Wakili Abel Ngilangwa. Vilevile, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maboresho ya Sheria na aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo mstaafu, Bw. Leonard Thadeo.













No comments:
Post a Comment