CCM KUANZA ZIARA YA KITAIFA KUSIKILIZA NA KUTATUA KERO ZA WANANCHI. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, January 17, 2026

CCM KUANZA ZIARA YA KITAIFA KUSIKILIZA NA KUTATUA KERO ZA WANANCHI.


Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA 


Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeendelea kuthibitisha kwa vitendo kuwa ni chama cha wananchi, baada ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) anayeshughulikia Itikadi, Uwenezi na Mafunzo, Kenani Labani Kihongosi, kutangaza kuanza kwa ziara ya kitaifa ya kichama itakayohusisha mikoa yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari leo katika Ukumbi wa Jakaya Convention Centre jijini Dodoma, Ndugu Kihongosi amesema ziara hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya chama, wananchi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), sambamba na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kusikiliza na kutatua kero za wananchi pamoja na kulinda amani, umoja na mshikamano wa Taifa.

Amesema kuwa CCM haiwezi kuendelea kuongoza kwa kutegemea taarifa za mezani pekee, bali ni lazima ishuke moja kwa moja kwa wananchi ili kupata uhalisia wa changamoto zao na kuzifanyia kazi kwa vitendo.

“Kama chama, tuna wajibu wa kwenda kuisimamia Serikali. CCM ni chama cha watu, na hatuwezi kuongoza kwa kusikia taarifa za mezani pekee. Lazima tushuke kwa wananchi, tusikilize kero zao na kuzitatua,” alisema Kihongosi.

Amefafanua kuwa CCM ni chama cha kijamii na kimaendeleo, kinachojengwa juu ya misingi ya amani, umoja, mshikamano na kulinda utu wa Mtanzania, misingi iliyokiwezesha kukiongoza Taifa kwa uthabiti na amani kwa muda mrefu.

Alisisitiza kuwa CCM haitajenga Taifa kwa misingi ya chuki wala migawanyiko, bali kwa maridhiano na kuheshimiana, akiongeza kuwa maslahi ya Taifa yatabaki kuwa kipaumbele kuliko maslahi binafsi au ya makundi.

Aidha, MNEC huyo amesema CCM imefurahishwa na hatua ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kufanya kikao cha kufungua mwaka na Mabalozi wa Tanzania kutoka nchi mbalimbali, akisema hatua hiyo imeongeza heshima ya Taifa kimataifa na kuwapa faraja wanachama wa CCM kote nchini.

Kupitia ziara hiyo, chama kitafanya tathmini ya kina ya utekelezaji wa ahadi za siku 100 za Rais, huku kikihakikisha maslahi ya wananchi yanalindwa na hayapotoshwi kwa namna yoyote.

Ndugu Kihongosi pia ametoa onyo kwa Watanzania kutokubali kujiunga au kuunga mkono makundi au vyama vya kisiasa vinavyopandikiza chuki, migawanyiko na siasa zisizo za maridhiano, akisisitiza kuwa historia ya Tanzania imejengwa juu ya misingi ya umoja, amani na kuheshimiana.

“CCM haitakubali kuona mtu au kikundi chochote kinachopotosha ukweli, kinachohujumu amani au kinachotaka kurudisha nyuma maendeleo ya Taifa letu,” alisisitiza.

No comments:

Post a Comment