DC MAYEKA ATOA ONYO KALI KWA WAVAMIAJI WA CHANZO CHA MAJI KIBAIGWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, January 29, 2026

DC MAYEKA ATOA ONYO KALI KWA WAVAMIAJI WA CHANZO CHA MAJI KIBAIGWA


Na Okuly Julius, OKULY BLOG
KIBAIGWA, Kongwa


Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Mayeka S. Mayeka, ametoa onyo kali kwa wananchi wanaovamia na kuendesha shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo katika chanzo cha maji cha Mbuyuni kilichopo Kibaigwa, akisisitiza kuwa ni marufuku kabisa kufanya shughuli zozote katika vyanzo vya maji na kwamba watakaokaidi agizo hilo watachukuliwa hatua za kisheria.


Akizungumza leo Januari 29, 2026 wakati wa uzinduzi wa zoezi la upandaji miti lililoandaliwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) katika chanzo hicho cha maji, Mhe. Mayeka amesema chanzo cha maji hakina siasa, hivyo Serikali haitasita kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wote watakaobainika kulima, kujenga au kuharibu mazingira ya eneo hilo.

Amesema upungufu wa maji ni tishio la kiusalama, hivyo suala la maji ni nyeti na linahitaji ulinzi wa pamoja kwa kushirikiana na wananchi wote. Amehimiza upandaji miti na utunzaji wa mazingira katika vyanzo vya maji ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji safi na salama kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Mhe. Mayeka ameongeza kuwa idadi ya watu Kibaigwa inaongezeka kwa kasi, hali inayoongeza mahitaji ya maji, hivyo uharibifu wa chanzo cha maji ni sawa na kuwanyima wananchi haki yao ya msingi ya kupata huduma ya maji.

Amesisitiza kuwa chanzo cha maji ni mali ya wananchi wote na si cha DUWASA, ambao ni wasimamizi tu, hivyo uharibifu wa miundombinu ya maji ni hujuma kwa jamii nzima.

Aidha, amesema uharibifu wa mazingira haukopeshi kwani madhara yake hujitokeza haraka, na kuwataka wananchi kuacha mara moja kuvamia eneo la chanzo cha maji, hususan wale waliendeleza majengo au shughuli nyingine kinyume cha sheria wakifahamu wazi kuwa eneo hilo lilitengwa mahsusi kwa ajili ya kuhifadhi chanzo cha maji.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mayeka amebainisha kuwa wananchi 24 tayari wamelipwa fidia ili kuondoka katika eneo la chanzo cha maji, huku akiwataka wananchi wanaoendelea kulima karibu na chanzo hicho kuacha mara moja, akisisitiza kuwa ni marufuku kabisa kufanya shughuli zozote za kibinadamu katika eneo hilo.

Amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua kali kwa wote watakaokiuka maagizo hayo ili kulinda rasilimali maji na kuhakikisha huduma ya maji inaendelea kupatikana kwa wananchi wa Kibaigwa na maeneo jirani.


Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa DUWASA, Bi. Rahel Muhando, amesema mamlaka hiyo inaendelea kutambua mchango mkubwa wa mazingira katika uhifadhi na uendelevu wa vyanzo vya maji, akisisitiza kuwa upandaji miti ni njia muhimu ya kuhakikisha vyanzo hivyo vinaendelea kutoa huduma kwa muda mrefu.

Ameeleza kuwa katika chanzo hicho cha maji pekee, miti 1,000 imepandwa, huku DUWASA ikilenga kupanda zaidi ya miti 4,500 katika vyanzo vyote vya maji vinavyohudumiwa na mamlaka hiyo, kwa lengo la kuvilinda na kuhakikisha vinakuwa na maji ya uhakika kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.

Bi. Muhando amewahimiza wananchi kuendeleza utamaduni wa kupanda na kutunza miti, hususan katika maeneo yanayozunguka vyanzo vya maji, ili kulinda rasilimali hiyo muhimu kwa maisha ya binadamu na maendeleo ya jamii.

“Uzalendo wa kweli ni kutunza mazingira. Kila mwananchi anapaswa kushiriki kikamilifu katika kupanda miti na kulinda vyanzo vya maji,” imeelezwa katika kauli ya DUWASA wakati wa zoezi hilo.

Zoezi hilo ni sehemu ya mikakati ya DUWASA kwa kushirikiana na Serikali ya Wilaya ya Kongwa ya kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama unaimarika sambamba na uhifadhi wa mazingira, kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

No comments:

Post a Comment