
Na Siximund Bagishe, Arusha.
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imetakiwa kuongeza bidi katika udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu kwa kuongeza matumizi ya teknolojia,vituo vya askari,vitendea kazi na kuimarisha ulinzi katika maeneo ya hifadhi ili kuongeza idadi ya watalii na mapato.
Akizungumza wakati wa kuzindua bodi mpya ya nne ya Mamlaka ya Usimamizi wa wanyamapori Jijini Arusha Januari 09,2026, Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Ashatu Kijaji ameielekeza bodi hiyo kujikita katika utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akizindua bungela 13, na kwamba utekelezaji wa maelekezo hayo yafanyike kwa ufanisi wa hali ya juu, na yajioneshe bila kutafutwa na yajidhihirishe katika maisha ya Watanzania ama kwenye mchango wa sekta ya utalii katika pato la Taifa.
Pia Dkt. Kijaji ameitaka bodi hiyo kuchukua hatua za kukomeshwa ama kupunguzwa kwa matukio ya migongano baina ya wanyamapori wakali na waharibifu,migogoro ya mipaka,uingizwaji wa mifugo hifadhini na kampeni za kupinga uwindaji haramu na ujangili.
Aidha, ameongeza kuwa mojawapo ya changamoto zinazoikabili TAWA ni pamoja na ukosefu wa miundombinu wezeshi ya utalii katika maeneo ya hifadhi ikiwemo barabara na madaraja, maeneo ya malazi na viwanja vya ndege hali inayoathiri uhifadhi na utalii na kuielekeza bodi hiyo kuweka mikakati itakayosaidia kutatua changamoto hizo.
Amesisitiza kuwa bodi hiyo itende kazi yake kwa kuzingatia utu kwa Watanzania wanaoishi kando ya hifadhi kwa kuzingatia maelekezo na maono ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kutaka anapomaliza awamu yake ya pili ya uongozi mwaka 2030 aondoke madarakani akiwa ameacha tabasamu kwa Watanzania.
Akizungumza wakati wa kumkaribisha Mhe Waziri, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Utalii katika Wizara ya Maliasili na Utalii Bwana Mabula Nkoba amesema Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia Mwenyekiti wa bodi hiyo Meja Jenarali Mstaafu Hamis Semfuko kuendelea na majukumu yake kwa kipindi cha pili na kuongeza kuwa bodi hiyo ina mchanganyiko wa wataalamu wenye uzoefu na wasomi kutoka nyanja za uhifadhi,ikolojia, ulinzi na usalama ambao watasaidia kukuza, kuendeleza na kutunza uhifadhi kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya bodi hiyo, Mwenyekiti wa bodi ya nne ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori nchini (TAWA) Meja Jenerali Mstaafu Hamis Semfuko amesema watatekeleza wajibu waliopewa kwa uzalendo,weledi, nidhamu,ubunifu na kwa kuzingatia utu ili kuenzi imani iliyooneshwa kwao na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuhakikisha TAWAinakuwa kinara katika uhifadhi, utoaji huduma na kufikia malengo ya kuanzishwa kwake



No comments:
Post a Comment