DKT. NCHEMBA: USHIRIKISHWAJI WA TAKUKURU KATIKA BAJETI NI MUHIMU KUDHIBITI RUSHWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, January 26, 2026

DKT. NCHEMBA: USHIRIKISHWAJI WA TAKUKURU KATIKA BAJETI NI MUHIMU KUDHIBITI RUSHWA




Na Shua Ndereka, Morogoro


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameisisitiza Ofisi ya Rais – Sekretarieti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuishirikisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) katika maandalizi ya bajeti, ili kuziba mianya yenye viashiria vya rushwa hususan katika maeneo nyeti yanayohusisha matumizi ya fedha za umma.

Akizungumza kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa uzinduzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wa TAKUKURU uliofanyika Januari 26, 2026 katika Ukumbi wa Cate Convention Centre, Manispaa ya Morogoro, Waziri Mkuu amesema kuwa kuziba mianya ya rushwa ni hatua muhimu ya kuzuia wachache kunufaika kwa kuchukua haki ya wenzao.

Amesema hatua hiyo itawezesha kila Mtanzania kunufaika na rasilimali za Taifa kwa usawa.

Waziri Mkuu amebainisha kuwa rushwa husababisha kukosekana kwa haki na usawa katika utumishi wa umma, ambapo baadhi ya watumishi hunufaika kinyume cha maadili huku wengine wakibaki wakihangaika licha ya kufanya kazi kwa uaminifu.

“Kuna watumishi ambao hawapo kwenye dirisha lolote la kupokea rushwa lakini wanapambana sana kumaliza mwezi, ilhali wanamuona mwenzao anaendelea kumea tu. Haya ni mambo ambayo hatupaswi kuyaonea aibu wala kuyanyamazia,” amesema Dkt. Nchemba.

Aidha, ameipongeza TAKUKURU na kuitaka ichukue hatua za haraka kuziba mianya ya rushwa hususan kwa watumishi wanaonufaika kwa njia zisizo halali, ili kuhakikisha huduma za jamii zinawafikia wananchi wote kwa haki, ikiwemo upatikanaji wa dawa hospitalini, miundombinu ya barabara, pamoja na fursa za mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi kutoka familia zisizojiweza.

Amesisitiza kuwa rushwa inadhalilisha utu wa binadamu na kudhoofisha utoaji wa huduma za jamii, hivyo amezitaka taasisi za Serikali kubaini na kuziba mianya ya rushwa katika maeneo ya manunuzi ya umma, utekelezaji wa miradi na usimamizi wa mikataba, akibainisha kuwa zaidi ya asilimia 75 ya bajeti ya Serikali hupita katika maeneo hayo.

Pia amesema Serikali iko tayari kufanya marekebisho ya kisheria na kiutawala pale itakapobainika kuwa kuna vikwazo vinavyoathiri utekelezaji wa majukumu ya TAKUKURU, huku viongozi wa taasisi hiyo wakitakiwa kuwasilisha mapendekezo yao bila kusita.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameipongeza TAKUKURU kwa kufanikiwa kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 60.2 ambazo zimerejeshwa Serikalini na kutumika kuboresha huduma za kijamii, ikiwemo ununuzi wa dawa hospitalini, upanuzi wa huduma ya umeme vijijini, upatikanaji wa maji safi na salama, pamoja na kuchangia elimu bila ada na mikopo ya elimu ya juu.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, amesema TAKUKURU ilifuatilia miradi ya maendeleo 619 yenye thamani ya shilingi bilioni 553.45 na kuokoa shilingi milioni 173.5 zilizokuwa hatarini kupotea kutokana na vitendo vya rushwa.

Ameongeza kuwa kati ya kesi 489 zilizokuwa zikiendeshwa mahakamani, Jamhuri ilishinda asilimia 68.8 ya kesi zilizotolewa maamuzi, ambapo washtakiwa walibainika kuwa na hatia.

“Ni imani yetu kuwa kiwango cha ushindi wa kesi kitaongezeka zaidi ifikapo Juni 2026,” amesema Chalamila.

Mkutano Mkuu wa TAKUKURU wa mwaka 2025 umehudhuriwa na jumla ya viongozi 234 kutoka Makao Makuu, mikoa, wilaya na vituo maalumu nchini, na unatarajiwa kuhitimishwa Januari 29, 2026.



No comments:

Post a Comment