Na Mwandishi Wetu- Dodoma
Serikali imesema ujenzi wa uwanja wa Mpira wa Miguu katika Manispaa ya Geita utaleta tabasamu kwa Watanzania walioko katika mkoa wa Geita pamoja na Wizara ya michezo kuuona kama sehemu ya viwanja vitakavyotumika katika mashindano ya AFCON 2027 kama utakamilika kwa wakati.
Hayo yameelezwa leo Januari 28,2026 Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Dkt. Jafar Seif wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Geita Mjini Mha. Chacha Wambura aliyehoji, Serikali kama haioni haja ya kufanya mapitio kwa haraka ili uwanja huo uweze kukamilika kabla ya kuanza mashindano ya AFCON 2027.
"Baada ya kumpata mkandarasi mshauri, tayari kiasi cha fedha cha bilioni 3.4 zimetengwa kwaajili ya ukamilishaji wa jukwaa kuu, majukwaa ya watazamaji na sehemu ya kuchezea mpira ambapo ikadiliwa kuwa ujenzi utakamilika ifikapo Oktoba 2026,"amesema.
Awali akijibu swali la msingi la Mbunge huyo juu ya hatua gani zimefikiwa katika kuandaa Mpango wa kuendeleza na kukamilisha ujenzi wa uwanja huo, Dkt. Seif amesema Serikali kwa kushirikiana na Mgodi wa Geita Mine imepata mkandarasi mshauri Ms NORPLAN ambaye amefanya mapitio ya gharama halisi za kukamilisha ujenzi wa uwanja huo na kiasi cha shilingi bilioni 5 zinahitajika.
"Aidha, Serikali inaendelea na mapitio ya gharama zilizowasilishwa na mkandarasi mshauri ili kuweza kuendelea na ujenzi kupitia fedha za CSR zitakazotengwa katika mwaka 2026/27,"amesema.
Ameongeza kuwa uwanja wa mpira wa miguu Geita ulianza kujengwa mwaka 2021 kwa kutumia fedha za uwajibikaji wa Kijamii wa Mashirika (CSR) kwa gharama ya shilingi bilioni 5.46 kupitia Mgodi wa Geita Gold Mine.
Hata hivyo, ujenzi ulisimama mwaka 2023 ukiwa asilimia 71, baada ya Mkandarasi Ms EFQ Co. Ltd kusitishiwa mkataba kutokana na mabadiliko ya kanuni ya miradi ya CSR.



No comments:
Post a Comment