
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, ametoa onyo kwa Watumishi wa Umma dhidi ya matumizi ya baruapepe binafsi katika mawasiliano ya shughuli za Serikali.
Amesema kuwa, watumishi wote wa Umma wanapaswa kutumia baruapepe rasmi za Serikali ili kulinda usalama wa taarifa Serikalini, kuongeza uwajibikaji, kuimarisha mifumo rasmi ya mawasiliano ya Serikali sambamba na kuzuia kuvuja kwa taarifa za Serikali.
Akizungumza mapema hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Pili ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Mhe. Kikwete amesema, matumizi ya barua pepe zisizo za Serikali yamekuwa chanzo cha hatari ya uvujaji na upotevu wa taarifa nyeti za Serikali.
Alibainisha kuwa, Serikali imewekeza katika miundombinu ya TEHAMA inayokidhi viwango vya usalama na inapaswa kutumiwa ipasavyo katika mawasiliano ya shughuli zote za Serikali, ili kudhibiti na kulinda usalama wa taarifa muhimu za nchi.
“Kuanzia sasa, serikali itakuwa na jicho la karibu sana kuangalia namna watumishi wa Umma wanavyopeana taarifa za Serikali kupitia baruapepe rasmi za Serikali na si vinginevyo, nitoe wito kwa viongozi na watumishi wote wa umma kutumia anuani za baruapepe rasmi kwa ajili ya mawasiliano ya shughuli zote za Serikali, alisisitiza Waziri Kikwete.
Alibainisha kuwa, barua pepe za Serikali zinatoa mazingira salama ya kuhifadhi kumbukumbu, kudhibiti hatari ya kuvuja kwa taarifa za serikali, usalama na ulinzi wa taarifa hizo kwa mujibu wa sheria na miongozo mbalimbali inayohusu usalama na utunzaji wa taarifa za Serikali, sambamba na uwajibikaji kwa watumishi wa umma katika kuzingatia misingi ya utunzaji wa taarifa za Serikali.
“Matumizi ya baruapepe zisizo rasmi yamesababisha baadhi ya nyaraka za Serikali kupotea na wakati mwingine kuhatarisha usalama na usiri wa taarifa hizo ndani ya serikali, tukiwa kama watumishi wa umma sote tunawajibika kulinda usalama wa taarifa za Serikali kwa kutumia baruapepe rasmi za Serikali”, alisema Mhe.Kikwete.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Eng. Benedict Ndomba, alisema kuwa e-GA itaendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi za umma ili kuzijengea uwezo katika matumizi ya mfumo wa Buruapepe Serikalini (GMS).
Alisema kuwa, takriban zaidi ya miaka 10 sasa, tangu kuanza kutumika kwa mfumo wa GMS na kuleta matokeo chanya ikiwemo kurahisisha mawasiliano ndani na nje ya taasisi pamoja na kuwezesha utekelezaji wa maamuzi kwa wakati.
“e-GA tunatoa msaada wa kiufundi kwa saa 24 kwa watumiaji wa mifumo mbalimbali ukiwemo GMS na tutaendelea kufanya hivyo, ili kuhakikisha mawasiliano ya Serikali yanakuwa imara muda wote kupitia mfumo huu wa GMS”, alisema Ndomba.


No comments:
Post a Comment