NAIBU WAZIRI KWAGILWA ARIDHISHWA NA UJENZI WA BARABARA UTIRI-MAHANDE MBINGA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, January 11, 2026

NAIBU WAZIRI KWAGILWA ARIDHISHWA NA UJENZI WA BARABARA UTIRI-MAHANDE MBINGA



Na Mwandishi Wetu, Mbinga


Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI anayeshughulikia Elimu, Mhe. Reuben Kwagilwa ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Utiri–Mahande katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga, mkoani Ruvuma.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani humo, Mhe. Kwagilwa amekagua barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 16 na kumuelekeza mkandarasi kuongeza idadi ya wafanyakazi, vifaa na muda wa kazi pindi mvua zitakapopungua, ili mradi ukamilike kwa wakati na kuwanufaisha wananchi.

Amesisitiza kuwa miradi ya kimkakati kama ujenzi wa barabara hiyo lazima isisimamiwe kwa umakini ili iwe chachu ya maendeleo kwa wananchi.

Aidha, Mhe. Kwagilwa ameongeza kuwa barabara hiyo itarahisisha shughuli za kiuchumi, hususan usafirishaji wa mazao mbalimbali yanayozalishwa katika maeneo ya Mbinga na hivyo kuchangia katika kukuza uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Silivester Chinengo, amesema mradi huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 16 umefikia asilimia 69 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika ifikapo Mei 29, 2026.


No comments:

Post a Comment