
Na WMJJWM – Dar es Salaam
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, ametoa wito kwa jamii kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kutoa taarifa za wahusika wa matukio ya ukatili dhidi ya watoto ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa haraka.
Dkt. Gwajima ameyasema hayo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, ambapo amechapisha picha na taarifa za matukio mawili tofauti ya ukatili dhidi ya watoto yaliyotokea nchini. Matukio hayo yanahusisha mtoto aliyefanyiwa ukatili ambapo, kwa mujibu wa mtoa taarifa mtuhumiwa wa tukio hilo ni baba yake mzazi, baada ya mtoto huyo kutuhumiwa na mama yake wa kambo kuwa ameiba iPad ya mtoto wa jirani na tukio la pili ni la tuhuma za ukatili wa kijinsia kwa watoto wa kiume kuingiliwa kinyume na maumbile ambapo, mtuhumiwa ni baba yao mzazi.
Akitoa mrejesho wa matukio hayo, Dkt. Gwajima amesema hatua za kisheria tayari zimeanza kuchukuliwa ikiwemo kuripoti matukio hayo katika vyombo vya usalama, hususan Jeshi la Polisi, pamoja na kushirikisha viongozi mbalimbali ili kuwabaini wahusika na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria. Ameongeza kuwa Maafisa Ustawi wa Jamii tayari wameanza kuwafuatilia watoto waliopata madhara ili kuhakikisha wanapatiwa msaada wa haraka wa kisaikolojia, kiafya na kijamii.
Aidha, Waziri Gwajima amepongeza jamii kwa kuendelea kutoa ushirikiano katika mapambano dhidi ya ukatili kwa kutumia mitandao ya kijamii kutoa taarifa kwa wakati. Katika hatua hiyo, amewapongeza waliotoa taarifa hizo @yerickonyerere, @jemedarisaid na @munalove100 kwa ujasiri wao wa kuripoti matukio hayo na kusaidia mamlaka kuchukua hatua. Pia ametoa wito kwa wananchi wengine kuendelea kuibua na kuripoti matukio yote ya ukatili yanapotokea.
Hata hivyo, Dkt. Gwajima ametoa onyo kali kwa wote wanaojihusisha na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, akisisitiza kuwa Serikali kwa kushirikiana na jamii haitavumilia vitendo hivyo. Amesema:
“Ukatili dhidi ya watoto tutaukomesha kwa nguvu ya ushirikiano wa jamii na Serikali. Kila tukio litakaloibuliwa na kuripotiwa mapema litachukuliwa hatua za haraka na ninawahakikishia kuwa kila anayemfanyia mtoto ukatili ataonja mkono wa sheria kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto.”
Hata hivyo, Waziri Gwajima ameitaka jamii kuwa wavumilivu wakati taarifa kamili kuhusu matukio hayo ikiandaliwa kwa uharaka ili kuwezesha kupatikana kwa mrejesho wa hatua stahiki zilizochukuliwa na mamlaka husika.

No comments:
Post a Comment