
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema Serikali inaendelea kuunga mkono juhudi za Taasisi ya Lalji Foundation katika kuimarisha sekta ya elimu na maendeleo ya kijamii, hususan katika kuhakikisha watoto wanapata elimu bora na jumuishi.
Akizungumza Januari 10, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya ugawaji wa vifaa kwa wanafunzi kutoka vituo vya kulea watoto yatima, Waziri Mkenda amesema Serikali inautambua na kuuthamini mchango wa taasisi hiyo katika ujenzi wa shule na utoaji wa misaada mbalimbali inayochochea maendeleo ya elimu nchini.
Ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kutoa elimu bila ada kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita, pamoja na kutoa mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wenye uhitaji ili kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa fursa ya elimu.
Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Dkt. Abubakar Zuber Ali Mbwana, ameipongeza Taasisi ya Lalji Foundation kwa jitihada za kutoa misaada kwa watoto yatima na wasiojiweza, akisisitiza kuwa ni matendo yenye thawabu kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.
Kwa upande wake Mlezi wa Taasisi hiyo Ndg. Mohsin Lalji amesema kuwa Taasisi imewazawadia watoto 400 wa shule za Msingi vifaa vya shule ikiwemo sare.
Ameongeza kuwa katika kuchangia juhudi za Serikali katika sekta ya elimu, Taasisi imechangia madawati 300 kwenye shule zenye uhitaji.




No comments:
Post a Comment