PROF. MKENDA AZINDUA UGAWAJI WA VIFAA SAIDIZI VYA KIDIJITALI VYENYE THAMANI YA SH. BILIONI 5.3 KWA WALIMU WENYE ULEMAVU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, January 5, 2026

PROF. MKENDA AZINDUA UGAWAJI WA VIFAA SAIDIZI VYA KIDIJITALI VYENYE THAMANI YA SH. BILIONI 5.3 KWA WALIMU WENYE ULEMAVU


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Profesa Adolf Mkenda, amezindua ugawaji wa vifaa vya kielimu na saidizi vya kidijitali kwa walimu, wakufunzi na walimu tarajali wenye ulemavu, vyenye thamani ya Shilingi bilioni 5.3.

Uzinduzi wa vifaa hivyo umefanyika Januari 5, 2026 jijini Dodoma, ambapo Prof. Mkenda amesema Serikali inaendelea kutekeleza sera na maboresho ya mitaala ili kuhakikisha elimu jumuishi inatolewa kwa ufanisi kwa wanafunzi na walimu wenye mahitaji maalum.

Amesema uwekezaji unaofanywa na Serikali umewezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum kupata elimu bora, sambamba na kuwawezesha walimu wenye ulemavu kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Waziri Mkenda amekumbusha msisitizo uliotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwamba utekelezaji wa maendeleo jumuishi utakwenda sambamba na uboreshaji wa miundombinu na upatikanaji wa vifaa maalum kwa wanafunzi na walimu wenye mahitaji maalum katika ngazi zote za elimu.

Vifaa vilivyozinduliwa ni pamoja na kompyuta mpakato 688, mashine za kidijitali za kurekodi sauti 377, tabuleti 196, mashine za kielektroniki za braille 19, emboza 6, mashine za kuongeza sauti 7 pamoja na seti 4 za vifaa vya kupima usikivu.

Vifaa hivyo vinasambazwa katika shule za msingi 309, shule za sekondari 629 na vyuo vya ualimu 10, kwa ajili ya kuwahudumia walimu, wakufunzi na walimu tarajali wenye mahitaji maalum katika halmashauri zote 184 nchini.

Waliofaidika na vifaa hivyo ni walimu wenye ulemavu wa viungo 342, wenye changamoto ya uoni 310, wenye uziwi 155, wenye ualbino 90, wenye usikivu hafifu 158, walimu tarajali 63 pamoja na wakufunzi 20 wenye ulemavu.








No comments:

Post a Comment