RAIS MWINYI AWASISITIZA WANANCHI KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, January 2, 2026

RAIS MWINYI AWASISITIZA WANANCHI KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewasisitiza Wananchi kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha mipango na miradi ya maendeleo inatekelezwa na kukamilika kwa wakati uliopangwa.

Rais Dkt. Mwinyi ametoa wito huo leo tarehe 02 Januari 2026 alipoweka jiwe la msingi la Mradi wa Ujenzi wa Daraja la Uzi Ng’ambwa pamoja na barabara zake, katika hafla iliyofanyika Uzi Ng’ambwa, Mkoa wa Kusini Unguja. Hafla hiyo ni sehemu ya shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema Serikali ina dhamira ya dhati ya kuwaletea Wananchi maendeleo katika nyanja zote za maisha, hivyo ni muhimu kwa Wananchi kuunga mkono juhudi hizo badala ya kuwepo kwa watu wachache wanaokwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Rais Dkt. Mwinyi ametoa kauli hiyo kufuatia kuwepo kwa baadhi ya Wananchi waliogoma kuchukua fidia zao ili kupisha ujenzi wa Barabara ya Uzi Ng’ambwa, hali iliyosababisha kuchelewa kwa utekelezaji wa mradi huo.

Kutokana na hali hiyo, Rais Dkt. Mwinyi amewaagiza Masheha, Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa kuhakikisha Wananchi wote ambao bado hawajachukua fidia zao wanafanya hivyo mara moja, ili sehemu iliyobakia ya barabara iweze kujengwa kwa wakati uliopangwa.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameonesha kuridhishwa na hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa Daraja la Uzi Ng’ambwa lenye urefu wa kilomita 2.2 pamoja na barabara zake zenye urefu wa kilomita 6.5, na kumtaka mkandarasi kukamilisha kwa haraka maeneo yaliyobakia ili Wananchi waanze kunufaika na mradi huo.

Akitoa taarifa ya kitaalamu ya mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Ali Said Bakari, amesema Daraja la Uzi Ng’ambwa lenye urefu wa kilomita 2.2 limejengwa na Kampuni ya CCECC kwa gharama ya Shilingi Bilioni 36, likiwa na uwezo wa kuhudumia magari yenye uzito wa hadi tani 60. Mradi huo pia unahusisha ujenzi wa barabara ya njia mbili yenye urefu wa kilomita 6.5 kwa kiwango cha lami.

No comments:

Post a Comment