REA NA TPDC WAKAMILISHA MRADI WA USAMBAZAJI WA GESI ASILIA MKOANI LINDI NA PWANI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, January 23, 2026

REA NA TPDC WAKAMILISHA MRADI WA USAMBAZAJI WA GESI ASILIA MKOANI LINDI NA PWANI


Kisemvule, Pwani


Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa pamoja wamekamilisha ujenzi wa Mradi mkubwa na wa kimkakati wa Kusambaza Gesi Asilia katika maeneo yaliyopitiwa na mkuza wa bomba la gesi katika mikoa ya Lindi na Pwani ambapo REA imefadhili na TPDC imejenga na kusambaza miundombinu hadi kwa mtumiaji wa mwisho (Mwananchi) ambapo hadi Mradi umekamilika, REA imetumia jumla ya shilingi bilioni 6.8 kugharamia Mradi huo.

Akizungumza na Wanahabari maara baada ya kuisha kwa zoezi la ukaguzi wa miundombinu ya Mradi huo eneo la Kisemvule mkoani Pwani, tarehe 22 Januari, 2026 (Alasiri) Mhandisi Emanuel Yesaya, Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji wa Miradi kutoka REA, amesema jumla ya kaya 530 tayari zimefikishiwa miundombinu ya Mradi huo, na kuongeza kuwa Mradi umetekelezwa kwa kusambaza mabomba ya gesi asilia ya ukubwa mbalimbali yenye urefu wa jumla ya kilomita 25 pamoja na kituo kidogo cha kupunguza mgandamizo wa gesi katika mkoa wa Pwani ambapo miundombinu ya kusambaza gesi asilia imefika hadi majumbani katika kata ya Vikindu, kijiji cha Kisemvule.

Mhandisi, Yesaya amesema miundombinu ya gesi asilia imesambazwa hadi kwenye nyumba za Wananchi walio katika wigo wa Mradi na kuongeza kuwa Wananchi wapo huru kutumia nishati hiyo kwa ajili ya kupikia ambapo itawalazimu kununua majiko ya gesi ili kuanza kufurahia matumizi ya gesi asilia.

“Mfumo wa gesi uliowekwa unamwezesha Mwananchi kununua gesi wakati wowote kupitia namba maalum ya malipo ya Serikali (Control number).” Amekaririwa, Mhandisi, Yesaya.

Aidha ametoa wito kwa Wananchi kutumia gesi asilia kwani ni nafuu akisisitiza kuwa matumizi ya nishati hiyo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa, amesema REA kwa kushirikiana na TPDC itaendelea kutoa elimu kwa Wananchi ili kuwawezesha kuelewa umuhimu wa kutumia nishati safi, hususan gesi asilia, kwa ajili ya kupikia.

Imeelezwa kuwa Mradi huo ulikamilika rasmi tarehe 4 Januari, 2026 katika mkoa wa Pwani ambapo Wananchi 222 kati ya 530 hadi tarehe 22 Januari, 2026 walikuwa wameunganishwa na huduma hiyo kwa kufungiwa mita na wameshanunua majiko kwa ajili kuanza kutumia gesi asilia.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiji cha Kisemvule, Bwana Omary Makunge, ameishukuru REA kwa kufadhili Mradi wa kusambaza gesi asilia hadi kwenye makazi ya Wananchi wa kijiji hicho.

Bwana Omary amesema REA na TPDC wameukamilisha rasmi Mradi huo Mwezi Januari, 2026 na tangu wakati huo Wananchi wamekuwa wakifurahia huduma hiyo ambayo ni salama, nafuu kwa hali zao za kiuchumi.

“Kijiji ndani ya muda mfupi, kimepiga hatua kubwa ya maendeleo kutokana na matumizi ya gesi asilia majumbani, maombi ya kuunganishwa na Mradi yameongezeka kutoka kwa Wananchi ambao hawakufikiwa na Mradi, iwapo fursa itapatikana, tunaiomba REA iendelee kufadhili ili Wananchi wengi zaidi wafikiwe na miundombinu ya gesi asilia.” Amekaririwa Bwana Omary.

Naye, Bi. Mwanahamisi Seif amesema matumizi ya mkaa yana gharama kubwa na huchukua muda mrefu zaidi kupika ikilinganishwa na gesi asilia, hali inayowafanya Wananchi wengi kubadili na kwenda kwenye matumizi ya nishati hiyo safi kama inavyohamasishwa na Serikali.

Kwa upande wake, Bi. Veronica Bonaventure amesema faida kubwa ya gesi asilia ni uwezo wa kununua wakati wowote inapokwisha, tofauti na nishati nyingine zinazowategemea (Mawakala); amesema aliwahi kununua mita za ujazo wa gesi asilia, saa 4 usiku kwa kutumia simu yake, akibainisha kuwa kama angewategemea (Mfanyabiashara) asingepata huduma kutokana na kufungwa kwa maduka na changamoto za kiusalama.

Naye, Bi. Mariam Rashid amesema kwa wananchi wenye kipato cha chini, gesi asilia ni msaada mkubwa kwani unaweza kuinunua hadi kwa shilingi 1,000 na kupika chakula kwa siku tatu (3).

No comments:

Post a Comment