
Na Witness Masalu- WMJJWM, Dodoma.
Serikali inathamini ustawi wa watoto nchini hususan wanaoishi katika mazingira magumu.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Vijana,Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Rahma Kisuo katika hafla ya ugawaji wa bima za afya kutoka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ikiwa ni sehemu utekelezaji wa mpango wa kurejesha rasilimali kwa jamii (CSR), Januari 15, 2026 katika makao ya Taifa ya Kikombo yaliyopo mkoani Dodoma.
Mhe. Rahma amesema tukio hilo ni juhudi za Serikali katika kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wake ikiwemo watoto.
“Leo tunakabidhi Bima za Afya kwa watoto 162 wanaolelewa katika kituo hiki ukiwa ni msaada wa gharama za matibabu kutoka mfuko wa fidia kwa wafanyakazi ambapo msaada huu utawawezesha watoto hawa kuwa na uhakika wa kupata matibabu kwa kipindi cha mwaka mmoja.” amesema Mhe. Rahma.
Aidha Mhe. Rahma ametoa wito kwa taasisi nyingine za Serikali pamoja na Mashirika binafsi kuiga mfano wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa kujitokeza kusaidia makundi mbalimbali yenye mahitaji maalum kama sehemu ya shukrani kwa jamii inayowazunguka.

Awali akizungumza Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mhandisi MaryPrisca Mahundi amefafanua kuwa watoto walio katika makao hayo ni wale waliokutana na changamoto mbalimbali za malezi ikiwemo ukatili, kufiwa na wazazi au walezi lakini vilevile kukosa uangalizi wa kifamilia.
“Leo tunashuhudia tukio hili muhimu la utekelezaji wa moja wapo wa afua za afya jambo ambalo litachangia katika kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto waliopo katika makao haya” amesema Mhe. MaryPrisca.

Kwa Upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju ameeleza kwamba makao hayo yana uwezo wa kutoa hifadhi kwa watoto 250 kwa pamoja na kwa sasa kuna watoto 188 ambapo toka yazinduliwe 2021 yameshatoa hifadhi kwa watoto 717.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Fidia kwa wafanyakazi (WCF) Dkt. John Mduma amesema wataendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum hususani Makao ya Taifa ya Kikombo kwa kadri watakavyoweza.



No comments:
Post a Comment