‎WAZIRI GWAJIMA AZINDUA SEKRETARIETI YA KITAIFA YA URATIBU WA MAJUKWAA YA UWEZESHAJI WANAWAKE KIUCHUMI ‎ - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, January 16, 2026

‎WAZIRI GWAJIMA AZINDUA SEKRETARIETI YA KITAIFA YA URATIBU WA MAJUKWAA YA UWEZESHAJI WANAWAKE KIUCHUMI ‎



‎Na Saidi Saidi WJJWM - Dodoma


‎Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amezindua rasmi Sekretarieti ya Kitaifa ya Uratibu wa Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Leo Januari 15, 2026 Jijini Dodoma, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni msingi muhimu wa kuimarisha uratibu, na kasi ya utekelezaji wa ajenda ya uwezeshaji wanawake kiuchumi nchini kwa mujibu wa Mwongozo wa Majukwaa Toleo la 2024.

‎Akizungumza kwa njia ya mtandao wakati wa uzinduzi huo, Waziri Gwajima amesema majukwaa ya uwezeshaji wanawake ni Ajenda ya kitaifa iliyoasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kuwapa wanawake fursa za kiuchumi, kuimarisha uwezo wao wa uzalishaji, kuongeza kipato cha kaya na kuchangia kikamilifu katika uchumi wa Taifa.

‎Waziri Dkt. Gwajima ameilekeza Sekretarieti hiyo kusimamia kikamilifu uratibu wa Wizara za kisekta, kuandaa mipango madhubuti, kufuatilia utekelezaji wa Mwongozo katika ngazi zote na kuhakikisha wanawake waliopo kwenye majukwaa wanaunganishwa na fursa za mitaji, masoko, mafunzo ya ujasiriamali na teknolojia.

‎“Natoa wito kwa waratibu wa mikoa na viongozi wa majukwaa kuhakikisha majukwaa yanahuishwa, mikutano inafanyika kwa mujibu wa Mwongozo na shughuli za majukwaa zinajumuishwa kwenye bajeti za mamlaka za Serikali za Mitaa” amesema Dkt. Gwajima

‎Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi amewataka viongozi na waratibu wote wa majukwaa hayo kuimarisha ushirikiano kwani ushirikiano ni nguzo muhimu ya kufanikisha utekelezaji wa majukwaa kwa ufanisi na kufikia malengo ya kitaifa ya kuinua uchumi wa wanawake na jamii kwa ujumla.

‎Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu, amesema Wizara kwa kushirikiana na viongozi na waratibu wa majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa maelekezo yote yaliyotolewa, ili majukwaa hayo yawe chombo madhubuti cha kuwawezesha wanawake kiuchumi.

No comments:

Post a Comment