SERIKALI KUSHIRIKIANA NA VYUO VIKUU KUIMARISHA UWAJIBIKAJI KATIKA UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA UMMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, January 21, 2026

SERIKALI KUSHIRIKIANA NA VYUO VIKUU KUIMARISHA UWAJIBIKAJI KATIKA UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA UMMA


Na Mwandishi wetu, Dodoma


Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, kupitia Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Serikali, imesaini Hati za Mashirikiano (MoU) na Vyuo Vikuu vinne ambavyo ni Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo Kikuu cha Usimamizi wa Fedha na Taasisi ya Uhasibu Tanzania kwa lengo la kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji na tathmini unaotumia ushahidi katika kupanga na kutekeleza sera, mipango, programu na miradi ya maendeleo.  


Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyofanyika leo Januari 21, 2026 jijini Dodoma, Katibu Mkuu Ofisi Waziri Mkuu (SBUU) Dkt. Jim Yonazi amesema kupitia mashirikiano hayo, Serikali na Vyuo Vikuu vitashirikiana katika kuimarisha uwezo wa wataalamu wa ufuatiliaji na tathmini, kufanya tathmini za pamoja za miradi ya maendeleo, kuendeleza tafiti bunifu na kuhakikisha maarifa yanayozalishwa vyuoni yanatumika kuboresha utendaji wa Serikali. 

"Serikali imesisitiza kuwa, mafanikio ya MoU hizo yatapimwa kwa utekelezaji wake, kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, yenye msisitizo wa matokeo yanayopimika na manufaa halisi kwa wananchi" ameongeza Dkt. Yonazi.

Awali, akizungumza kwa niaba ya Makamu Wakuu wa Vyuo Vikuu vilivyoshiriki hafla, hiyo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma Prof. Lughano Kusiluka amesema kuwa, Ufuatiliaji na Tathmini ni eneo muhimu kwa ajili ya maendeleo ya taifa na Vyuo Vikuu vinaahidi kushirikiana na serikali katika kuhakikisha tunafanya vizuri katika eneo hilo ili nchi zinazotuzunguka wajifunze kutoka Tanzania.


Aidha, Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Serikali Bi. Sakina Mwinyimkuu amesema kuwa ushirikiano huo wenye nia ya pamoja una malengo ya kuongeza nguvu ya kusaidia taifa na kujenga tamaduni ya uwajibikaji.

No comments:

Post a Comment