
Na Mwandishi wetu, DSM
Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Philipo Sanga, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeweka msingi imara unaorejesha matumaini kwa vijana waliokatiza masomo ya Sekondari kutokana na changamoto mbalimbali za maisha.
Akizungumza katika kipindi cha “Morning Trumpet” kilichorushwa na UTV leo asubuhi (Januari 2, 2026), Prof. Sanga alieleza kuwa kupitia Waraka Na. 2 wa mwaka 2021 uliotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST) hivi sasa vijana wa jinsia zote wenye umri kuanzia miaka 13 – 21 waliokatiza masomo ya Sekondari kwa sababu mbalimbali wanayo fursa ya kuendelea na masomo.
Kulingana na Kiongozi huyo, Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ndiyo iliyopewa jukumu la kuwawezesha vijana hao kuendelea na masomo yao bure kupitia vituo vyake vilivyoko mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.
“TEWW kupitia mradi wa kuimarisha ubora wa elimu ya Sekondari kwa njia mbadala (SEQUIP-AEP) unaotekelezwa na WyEST kwa kushirikiana na Benki ya Dunia hivi sasa tunasajili vijana hao waliokatiza masomo ili waendelee na masomo bure katika vituo vyetu,” amesema Prof. Sanga.
Ametoa wito kwa vijana hao waliokatiza masomo kujiandikisha katika vituo vya TEWW vilivyopo karibu nao kwa ajili ya kuendelea na masomo yao ifikapo Januari 19, 2026, na kwamba kwa taarifa zaidi wanaweza kuwasiliana na Mratibu kwa Na. 0766 968 470 au kutembelea tovuti ya Taasisi: www.iae.ac.tz.

No comments:
Post a Comment