
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, akizungumza na waandishi wa habari, Januari 31,2026 jijini Dodoma, ppwakati akielezea utekelezaji wa ahadi ya siku 100 za Serikali ya Awamu ya Sita, kipindi cha pili cha uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika sekta ya Elimu.
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Jumla ya walimu, wakufunzi na walimu tarajali 1,055 kutoka Halmashauri 104 nchini wamenufaika na vifaa vya kidijiti na saidizi vyenye thamani ya Shilingi bilioni 5.4 vilivyonunuliwa na Serikali kwa lengo la kuboresha ujifunzaji na ufundishaji kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Akizungumza na waandishi wa habari Januari 31, 2026, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, wakati akielezea utekelezaji wa ahadi ya siku 100 za Serikali ya Awamu ya Sita, kipindi cha pili cha uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika sekta ya Elimu.
Prof. Mkenda amesema kuwa vifaa vilivyosambazwa vinajumuisha kompyuta mpakato 680, vifaa tisa vya Brain Note Touch Pass, voice recorder 377, tablets 196 kwa walimu wanaotumia lugha ya alama, mashine 30 za Perkins Braille, vifaa 101 vya kusaidia kusikia pamoja na mashine za Everest Drill Embosser.
Ameeleza kuwa mashine za Everest Drill Embosser zinawezesha walimu wasioona kuchapa maandishi kwa kutumia nukta nundu (Braille) na kuchapisha maandishi ya kawaida yanayoweza kusomwa na wanafunzi wengine, hivyo kuimarisha ujumuishaji katika mazingira ya elimu.
Amebainisha kuwa mpango huo ni mwendelezo wa juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalum wanajisikia kuwa sehemu ya jamii na hawatengeki na wanafunzi wengine. Kila mwaka Serikali imekuwa ikigawa vifaa saidizi pamoja na vitabu vinavyochapishwa kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita.
Aidha, Prof. Mkenda amesema vitabu vyote vinavyoandaliwa na Serikali kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) hutolewa pia katika matoleo maalum, ikiwemo vitabu vyenye maandishi makubwa kwa wenye uoni hafifu na vitabu vya nukta nundu (Braille) kwa wasioona kabisa.
Katika hatua nyingine, amesema utekelezaji wa ahadi za Rais Samia unaenda sambamba na upanuzi wa fursa za elimu ya juu kupitia utoaji wa mikopo na ujenzi wa miundombinu, ambapo Tanzania inaendelea kujenga kampasi mpya 16 za vyuo vikuu katika mikoa ambayo awali haikuwa na kampasi hizo.
Ameongeza kuwa mikoa yote nchini tayari ina vituo vya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, huku ujenzi wa kampasi mpya ukiendelea katika mikoa ya Kigoma, Kagera na Lindi ikiwemo kampasi za MUHAS na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo jiwe la msingi tayari limewekwa.

No comments:
Post a Comment