
Na Okuly Julius, OKULY BLOG - Dodoma
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amesema katika siku 100 za kwanza za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi chake cha pili cha uongozi, Wizara hiyo imefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya Shilingi milioni 821.7, hatua iliyochangia kuanzishwa kwa viwanda vidogo na kuzalisha ajira 546 za moja kwa moja, zikiwemo ajira 436 kwa vijana.
Waziri Kapinga ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa ahadi za Rais Samia katika sekta ya Viwanda na Biashara ndani ya siku 100 za kwanza za Awamu ya Sita katika kipindi cha pili cha uongozi wake.
Amesema Serikali imepiga hatua kubwa katika uendelezaji wa mitaa ya viwanda, baada ya kukamilisha tathmini ya awali ya kongani za viwanda katika mikoa 11 nchini, pamoja na kuandaa maeneo manne ya Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) kwa ajili ya uzinduzi rasmi, hali iliyoanza kuzalisha maelfu ya ajira, nyingi zikiwa ni za vijana.
“Uendelezaji wa mitaa ya viwanda ni mkakati mahsusi wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kupeleka viwanda karibu na wananchi, hususan vijijini na pembezoni mwa miji, ili kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, kukuza kipato cha wananchi na kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana,” amesema Kapinga.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, tathmini ya kongani na mitaa ya viwanda imefanyika katika mikoa ya Manyara, Singida, Mbeya, Iringa, Shinyanga, Ruvuma, Morogoro, Kilimanjaro, Dodoma, Tabora na Kigoma, ambapo maeneo hayo yamebainika kuwa na fursa kubwa za kuanzisha viwanda vya kuchakata mazao mbalimbali ikiwemo mpunga, alizeti, samaki, muhogo, mazao ya misitu, ngozi, pamoja na bidhaa za useremala na vyuma.
Ameeleza kuwa maeneo manne ya SIDO yaliyokamilika na yako tayari kwa uzinduzi rasmi ni SIDO Kigoma, Morogoro, Mbeya na Singida, ambayo tayari yameanza kuwavutia wajasiriamali na wawekezaji wadogo, huku yakitoa ajira na fursa za kujiajiri kwa vijana kupitia viwanda vidogo na vya kati.
Katika hatua nyingine, Waziri Kapinga amesema Serikali imeandaa Programu Maalum ya Uwekezaji kwa Vijana, inayolenga kuwezesha zaidi ya biashara 100,000 zinazoongozwa na vijana, kupitia ufadhili jumuishi, miundombinu ya viwanda, mafunzo ya ujasiriamali na upatikanaji wa masoko ya ndani na kimataifa.
Ameongeza kuwa kupitia programu hiyo, Serikali inalenga kuanzisha zaidi ya viwanda 9,000 na kuzalisha ajira zaidi ya milioni 6.5 ndani ya miaka sita, hatua itakayochangia kwa kiasi kikubwa kuboresha maisha ya vijana na kukuza uchumi wa taifa.
Waziri Kapinga amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha sera, miundombinu na mazingira ya uwekezaji, ili kuhakikisha mitaa ya viwanda inakuwa chachu ya uchumi shindani na maendeleo endelevu kwa Watanzania.

No comments:
Post a Comment