
Na Mwandishi Wetu - Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Madini imeanza maandalizi ya kulifanya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuwa mwekezaji mkubwa wa uchimbaji wa madini nchini, hatua inayolenga kuongeza tija na mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa Taifa.
Hayo yamesemwa leo Januari 16, 2026 na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kilichofanyika Bungeni jijini Dodoma.
Waziri Mavunde amesema STAMICO tayari imenunua mitambo mikubwa ya kisasa yenye uwezo wa kufanya uchimbaji mkubwa wa madini, jambo litakaloliwezesha Shirika hilo kuingia kwenye uchimbaji wa kiwango kikubwa sawa na migodi mikubwa kama Barrick Gold na Geita Gold Mine.
“Serikali inaijenga STAMICO kuwa mdau mkubwa wa uchimbaji wa madini ili kuongeza tija katika mnyororo mzima wa sekta ya madini na kuhakikisha Watanzania wananufaika zaidi na rasilimali zao,” amesema Mavunde.
Amesisitiza kuwa, sekta ya madini ni miongoni mwa sekta muhimu katika kukuza uchumi wa Taifa ambapo mafanikio yaliyopatikana yametokana na uongozi thabiti wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyoweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Akitoa taarifa ya Muundo na Majukumu ya STAMICO, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Dkt. Venance Mwasse, amesema Shirika hilo limeendelea kuimarika kutokana na hatua za makusudi zilizochukuliwa na Serikali ikiwemo kuimarisha uongozi, kutoa fedha za uwekezaji na kufanya usimamizi wa karibu.
Akitoa taarifa kwa Kamati hiyo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, amesema Mwaka 2024/25 Tume ya Madini ilipangiwa kukusanya Shilingi trilioni 1 na kufanikiwa kukusanya asilimia 108 ya lengo hilo. Kwa mwaka huu wa fedha, Tume imepangiwa kukusanya Shilingi trilioni 1.2 na hadi Desemba 2025 imekusanya asilimia 56.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu, amempongeza Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, pamoja na timu yake kwa usimamizi madhubuti na ufanisi mkubwa katika kuisimamia sekta ya madini.
Aidha, ameahidi kuwa Kamati hiyo itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa Wizara ya Madini na Taasisi zake ili kuhakikisha utekelezaji wa mipango na mikakati ya sekta hiyo unafanikiwa kwa manufaa ya Taifa.

No comments:
Post a Comment