
Na Shua Ndereka,OKULY BLOG - Morogoro
Msemo usemao “ukiwagusa wahitaji, umemgusa Mwenyezi Mungu” ni kiini cha mafundisho ya dini, hususan Ukristo na Uislamu, yanayohimiza huruma, upendo na kuwasaidia wenye mahitaji maalum katika jamii.
Katika Ukristo, maneno ya Yesu Kristo kwa wanafunzi wake yanasisitiza wazi wajibu huo, aliposema: “Kwa maana chochote mlichomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi” (Mathayo 25:40). Mafundisho haya yanawahimiza waumini kuwasaidia maskini, kuwafariji wagonjwa na kuwajali walio katika mazingira magumu.
Vivyo hivyo, katika Uislamu, Qur’an na Hadith vinahimiza sana kuwajali wahitaji. Qur’an inasema: “Na wafanyeni wema wazazi, jamaa, mayatima na masikini…” (Qur’an 4:36), huku Mtume Muhammad (SAW) akisema: “Mwenye kuwahurumia watu, Mwenyezi Mungu atamhurumia” (Hadith – Bukhari na Muslim).
Maudhui ya mafundisho hayo, yamejitokeza kwa vitendo kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ambayo imewagusa watoto njiti nchini, kwa kutoa msaada wa mashine maalum mbili za kuongeza joto kwa watoto hao.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya TAKUKURU kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wa Taasisi hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila, amesema viongozi na watumishi wa taasisi hiyo wamefanya matendo ya huruma kwa jamii kwa kugusa hospitali tisa za rufaa nchini.
Ikumbukwe kuwa, watoto njiti ni wale wanaozaliwa kabla ya kutimiza wiki 37 za ujauzito (miezi tisa kamili), na kwa sababu miili yao huwa haijakomaa kikamilifu, wanahitaji msaada wa joto maalum mara tu wanapozaliwa.
“Mashine hizi ni New Radiant Warmer na Neonatal Resuscitation System ambazo zitasaidia kuwapa watoto njiti joto na kupunguza madhara ya homa ya manjano…Mashine hizo zimenunuliwa kupitia michango binafsi ya watumishi wa TAKUKURU,” amesema Chalamila.
Chalamila amesema, tayari TAKUKURU imegusa hospitali za rufaa katika mikoa ya Arusha, Ruvuma, Njombe, Mbeya, Songwe, Dodoma, Rukwa, Katavi na Pwani ikiwa wiki hii taasisi hiyo inatarajia kukabidhi mashine hizo, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro huku wiki ijayo ikitarajiwa kufikisha msaada huo katika mikoa ya Tanga na Kilimanjaro.
Amebainisha kuwa, lengo la TAKUKURU ni kufikia hospitali zote za rufaa nchini ili kuimarisha afya za wananchi, akisisitiza kuwa mapambano dhidi ya rushwa yanahitaji nguvu kazi thabiti, yenye afya njema na ustawi wa jamii kwa ujumla.
Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wa TAKUKURU unaendelea mkoani Morogoro hadi Januari 29, 2026, ambapo ulizinduliwa rasmi jana Januari 26, 2026, na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.



No comments:
Post a Comment