
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema kiasi cha Sh. Bilioni 6,02 kinatarajiwa kuwalipwa na serikali kwa wananchi 347 wa Vijiji vya Lifua, Liugai na Masimavalafu wilayani Ludewa, Mkoa wa Njombe, waliopisha utekelezaji wa mradi wa umeme, katika mwaka wa fedha 2026/27.
Aidha, amesema kuwa hadi kufikia Desemba 2025, zoezi la uthamini wa fidia kwa wananchi hao limekamilika na kwa sasa lipo tayari kwa hatua ya uhakiki na uwekaji wazi wa jedwali la wafidiwa.
Waziri Ndejembi ametoa kauli hiyo leo Januari 27, 2026, bungeni jijini Dodoma katika kikao cha kwanza cha Mkutano wa Pili wa Bunge la 13, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Ludewa, Mhe. Joseph Kamonga, ambaye amehoji ni lini fidia kwa wananchi wa Kijiji cha Liugai, Kata ya Luilo, italipwa ili kupisha mradi wa umeme.
Akijibu swali hilo, Mhe.Ndejembi ameliambia Bunge kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha uhakiki na ulipaji wa fidia unafanyika kwa uwazi na kwa wakati, ili wananchi wanufaike kikamilifu na mradi huo muhimu wa nishati.

No comments:
Post a Comment