NAIBU WAZIRI SALOME AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KATIKA WIKI YA NISHATI INDIA 2026 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, January 27, 2026

NAIBU WAZIRI SALOME AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KATIKA WIKI YA NISHATI INDIA 2026


Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, leo Januari 27, 2026 ameshiriki katika ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Nishati India (India Energy Week – IEW 2026), yanayolenga kujadili na kuweka mikakati ya pamoja ya kukuza sekta ya nishati kwa njia endelevu na shirikishi, sambamba na kubainisha fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika nchi washirika pamoja na namna bora ya kuzifikia.

Maadhimisho hayo yamefunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi, katika Jimbo la Goa nchini India, na yanahudhuriwa na washiriki kutoka zaidi ya nchi 125 duniani, wakiwemo viongozi wa serikali, wataalamu wa nishati, wawekezaji na wadau wa sekta binafsi.

Katika maadhimisho hayo, Mhe. Salome ameambatana na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini India, Mhe. Balozi Anisa Mbega, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Dkt. James Andilile, Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Umeme kutoka Wizara ya Nishati, Mha. Styden Rwebangila, pamoja na wataalamu wengine kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA).

Ushiriki wa Tanzania katika IEW 2026 unaakisi dhamira ya Serikali ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kuvutia uwekezaji katika sekta ya nishati, pamoja na kubadilishana uzoefu na teknolojia zitakazochochea maendeleo endelevu ya sekta hiyo nchini. ‎

No comments:

Post a Comment