
Na OWM TAMISEMI – Dodoma
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Seikali za Mitaa (OWM- TAMISEMI) imekamilisha maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wa elimu ya awali, Darasa la Kwanza na Kidato cha Kwanza kwa mwaka 2026 na kuwataka Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, viongozi wa Halmashauri kushirikiana na wadau wa elimu ili kuhakikisha wanafunzi wote wakiwemo wenye mahitaji maalum, wanaanza masomo Januari 13, 2026 bila vikwazo vyovyote.
Taarifa hiyo imetolewa leo Januari 9, 2026 na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini OWM -TAMISEMI Bi. Roida Andusamile ambaye amebainisha kuwa zaidi ya Shilingi Bilioni 196.7 zimetumika kujenga shule mpya, madarasa ya elimu ya awali, msingi na maalum pamoja na matundu ya vyoo.
Aidha, zaidi ya Shilingi Bilioni 14.1 zimetumika kuandaa miundombinu itakayowezesha shughuli za ufundishaji na ujifunzaji katika shule za msingi.
Bi. Andusamile amesema, kwa mujibu wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 Toleo la 2023, watoto wenye umri wa miaka sita wanapaswa kuandikishwa Darasa la Kwanza, huku takwimu zikionesha kuwa jumla ya watoto zaidi ya milioni 1.9 wanatarajiwa kuanza elimu ya msingi mwaka 2026.
Bi. Andusamile amesisitiza kuwa, Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya elimu kupitia ujenzi wa shule mpya, madarasa, vyoo, maabara, shule za amali na ununuzi wa vifaa vya TEHAMA, ambapo zaidi ya Shilingi Bilioni 283 zimetumika.
Kwa upande wa elimu ya sekondari, Bi. Andusamile amesema Serikali ilitoa zaidi ya Shilingi Bilioni 28.4 kama ruzuku ya uendeshaji wa shule hizo, ili ziweze kuwahudumia wanafunzi 937,581, wakiwemo wenye mahitaji maalum 3,228 ambao walipangiwa shule kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi wa wanafunzi wa Kidato cha Kwanza yaliyotangazwa Desemba 04, 2025.
Aidha, Bi. Andusamile amesisitiza kuwa, OWM - TAMISEMI inawakumbusha wananchi kuzingatia Waraka wa Elimu Namba 3 wa mwaka 2016 kuhusu utekelezaji wa Elimu Msingi Bila Malipo, ambao unabainisha majukumu ya kila mdau tatika kuhakikisha wanafunzi wanaripoti shuleni na kupata elimu bora.



No comments:
Post a Comment