TANFORD YATANGAZA KONGAMANO LA KIMATAIFA LITAKALOFANYIKA DUBAI MWAKA HUU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, January 28, 2026

TANFORD YATANGAZA KONGAMANO LA KIMATAIFA LITAKALOFANYIKA DUBAI MWAKA HUU



Umoja wa Wawakilishi wa Mawakala wa Usafirishaji wa Mizigo wa Tanzania waliopo Dubai ujulikanao kama Tanzania Freight Forwarders Representation in Dubai (TANFORD), umeandaa kongamano la siku mbili litakalofanyika katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), jijini Dubai, kwa lengo la kuinadi Tanzania katika masoko ya kimataifa na kufungua fursa za biashara kwa wafanyabiashara wa Kitanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa TANFORD, Bw. Hussein Jamal, amesema kongamano hilo lijulikanalo kama Tanzania Trade and Logistics Forum 2026, litafanyika tarehe 13 na 14 Februari, 2026, na linatarajiwa kuwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya biashara na usafirishaji ili kuimarisha mahusiano ya kibiashara kati ya Tanzania na Dubai.

Bw. Jamal amesema lengo la kongamano hilo ni kuitangaza Tanzania kimataifa na kuifanya kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji katika Afrika Mashariki na Kati, sambamba na kukuza matumizi ya bandari na miundombinu ya usafirishaji ya Tanzania kwa kukusanya mizigo kutoka masoko ya kimataifa kupitia nchi hiyo.

Ameeleza kuwa kongamano hilo pia litasaidia kufungua masoko mapya ya bidhaa za Kitanzania kwa kuwakutanisha wafanyabiashara wa ndani na wateja wa kimataifa watakaoshiriki katika mkutano huo.

“TANFORD inasimama kama daraja la kibiashara kati ya Tanzania na masoko ya kimataifa, kwa lengo la kuwasaidia Watanzania kutambua na kutumia fursa za biashara na usafirishaji zilizopo Dubai, pamoja na kutangaza biashara zao kimataifa,” amesema Bw. Jamal.

Ameongeza kuwa kongamano hilo ni fursa adhimu kwa wadau wa sekta binafsi, taasisi za serikali na makampuni ya usafirishaji, kwani litatoa manufaa kwa mtu mmoja mmoja, makampuni na taifa kwa ujumla.

Taasisi zinazotarajiwa kushiriki katika kongamano hilo ni pamoja na TPA, TRA, DP World, TAFFA, TANTRADE, TATOA, Port Marine Clearing & Forwarding, Silent Ocean, Kilimanjaro Star Cargo, pamoja na TPSF.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE, Dkt. Latifa Mohammed Khamis, amesema kuwa kushiriki katika makongamano ya kimataifa ni muhimu kwani husaidia kujenga mahusiano bora kati ya wafanyabiashara wa ndani na wa kimataifa.

Amesema, “Nawasihi wafanyabiashara wa Kitanzania kushiriki kongamano hili kwani litafungua fursa za ushirikiano na wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali.”

Naye Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Bw. Edwin Urio, amesema kuwa kongamano hilo ni fursa ya kujitangaza kibiashara, kujijengea uwezo na kuchangia kukuza uchumi wa taifa.

Ameeleza kuwa sekta ya logistics na usafirishaji ndiyo iliyoongoza kwa kuingiza fedha za kigeni nchini katika mwaka wa fedha 2024/2025, na imeendelea kuwa uti wa mgongo wa ukuaji wa uchumi wa taifa lolote.

Bw. Urio pia amepongeza taasisi za serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi katika kuandaa kongamano hilo, akisema ushirikiano huo una manufaa makubwa kwa maendeleo ya uchumi wa Tanzania.



No comments:

Post a Comment