TANZANIA YASISITIZA UONGEZAJI THAMANI MADINI BARANI AFRIKA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, January 15, 2026

TANZANIA YASISITIZA UONGEZAJI THAMANI MADINI BARANI AFRIKA


Riyadh, Saudi Arabia


Tanzania imetambua shughuli za uongezaji thamani madini kama nguzo muhimu ya kuleta maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii lengo kubwa ikiwa ni kuondokana na uuzaji na usafirishaji wa madini ghafi kwa nchi zinazozalisha madini mbalimbali Barani Afrika.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Madini Mhe. Dkt. Steven Kiruswa, wakati akizungumza kwenye Kongamano la Kimataifa la Madini lijukanalo kama Future Minerals Forum 2026 lililowakutanisha mawaziri, viongozi mashuhuri na wadau wa sekta ya madini kutoka zaidi ya nchi 100 ndani na nje ya Bara la Afrika. 

Dkt. Kiruswa amesema kuwa, rasilimali madini ni moja ya utajiri mkubwa uliopo Barani Afrika hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuweka mkazo katika shughuli za uongezaji thamani madini ndani ya nchi za Afrika ambapo kama kila nchi itazingatia hilo itakuwa moja ya ufunguo wa kubadilisha utajiri wa madini kuwa kichocheo cha maendeleo endelevu kwa wananchi na taifa kwa ujumla. 

Akielezea kuhusu juhudi mbalimbali zinafanywa na Serikali ya Tanzania katika kuendeleza Sekta ya Madini, Dkt. Kiruswa ameeleza kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea kuboresha miundombinu ya usafirishaji na mawasiliano ikiwemo ujenzi wa reli ya mwendo kasi, barabara, nishati ya umeme na uongezaji wa bandari ili kuhakiskisha rasilimali zinasafirishwa kwa urahisi kutokea mgodini na kiwandani.

Dkt. Kiruswa amefafanua kuwa, ili kufanikisha hilo ni vyema kila taifa liendeleze viwanda vya uchakataji, uchenjuaji na usafishaji madini akitolea mfano kwa taifa la Tanzania linavyoendeleza juhudi mbalimbali katika mnyororo wa thamani madini ikiwemo kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, mifumo ya usafirishaji katika ngazi ya kimataifa kupitia Bandari ya Dar es Salaam.

Akisisitiza kuhusu Ushirikiano wa kikanda, Dkt. Kiruswa amesisitiza kuwa, ndani ya Bara la Afrika tunapaswa kushirikiana kwa kuanzisha vituo vya kikanda vya uchenjuaji, uchakataji na usafishaji madini katika nchi zenye miundombinu mizuri ili nchi jirani pia ziweze kuvitumia ikiwa pamoja na kujenga mahusiano ya kisekta kati ya Afrika na Muungano wa kiuchumi na kikanda kati ya nchi za Afrika na nchi za Mashariki ya Kati.

Katika Kongamano hilo la Kimataifa Tanzania imewakilishwa na Naibu Waziri wa Madini, Kaimu Balozi, Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Riyadh- Saudi Arabia pamoja na wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Madini, Tume ya Madini, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST)

No comments:

Post a Comment