TUME YA MADINI YAANGAZIA FURSA ZA UWEKEZAJI MAONESHO YA KIMATAIFA ZANZIBAR - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, January 7, 2026

TUME YA MADINI YAANGAZIA FURSA ZA UWEKEZAJI MAONESHO YA KIMATAIFA ZANZIBAR



Na Mwandishi Wetu, ZANZIBAR


Tume ya Madini kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali na sekta binafsi inashiriki kikamilifu katika Maonesho ya 12 ya Biashara ya Kimataifa Zanzibar yanayoendelea katika eneo la Fumba, Zanzibar, kwa lengo la kutangaza fursa lukuki za uwekezaji zilizopo katika sekta ya madini nchini.

Maonesho hayo yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Kujenga Ukuaji Jumuishi Kupitia Biashara na Ubunifu,” ambapo Tume ya Madini imeweka mkazo katika kuonesha fursa za utafiti wa madini, uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini, pamoja na utoaji wa huduma na bidhaa kwenye migodi.

Katika banda la Tume, wananchi wengi wa Zanzibar wamejitokeza kupata elimu kuhusu mchango wa sekta ya madini katika maendeleo ya taifa, hususan katika kuongeza pato la Taifa, ajira na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja.

Wataalam wa Tume wameeleza mwelekeo wa Tanzania katika kuimarisha uchimbaji endelevu wa madini na kuongeza thamani ya rasilimali hizo, sambamba na sera, kanuni na mifumo rafiki iliyowekwa ili kuwawezesha wananchi na wawekezaji kushiriki kikamilifu katika sekta hiyo.

Akizungumza katika mahojiano maalum, Meneja wa Mahusiano kwa Umma na Mawasiliano wa Tume ya Madini, Greyson Mwase, amesema lengo kuu la ushiriki wa Tume katika maonesho hayo ni kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna wanavyoweza kushiriki moja kwa moja katika mnyororo wa thamani wa madini na kunufaika kiuchumi.

“Sekta ya madini si kwa wawekezaji wakubwa pekee. Kuna fursa nyingi kwa wachimbaji wadogo, wajasiriamali, vijana na wanawake kushiriki kupitia uchimbaji mdogo, uchenjuaji, biashara ya madini, pamoja na utoaji wa bidhaa na huduma kwenye migodi,” amesema Mwase.

Ameongeza kuwa Tume inawahamasisha wananchi kuomba Leseni za Uchimbaji Mdogo wa Madini (PMLs), kuanzisha viwanda vidogo vya kukata na kung’arisha madini (lapidaries), pamoja na shughuli za uchenjuaji wa madini ya dhahabu, vito vya thamani na madini ya viwandani ili kuongeza thamani kabla ya kuyapeleka sokoni.

Aidha, Mwase amesisitiza umuhimu wa kutumia masoko na vituo vya ununuzi wa madini vilivyoanzishwa nchini, ambavyo huwezesha wachimbaji na wafanyabiashara kuuza madini yao kwa uwazi na kwa kuzingatia bei elekezi za kila siku zinazotolewa na Tume kulingana na mwenendo wa Soko la Dunia.

Kuhusu ushiriki wa Watanzania katika utoaji wa huduma kwenye migodi, amesema Tume inatekeleza kikamilifu Kanuni za Ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini, zinazolenga kuhamasisha ajira kwa Watanzania, ununuzi wa bidhaa na huduma za ndani, pamoja na uhamishaji wa ujuzi na teknolojia.

“Huduma za upishi, usafirishaji, usambazaji wa mafuta, ujenzi, ulinzi na nyinginezo ni fursa kubwa kwa Watanzania. Tunawahimiza wasajili biashara zao, wapate vibali vinavyotakiwa na waongeze uwezo wao wa kiufundi ili kunufaika zaidi,” ameeleza.

Amebainisha pia kuwa vijana wa Kitanzania wanayo nafasi kubwa ya ajira na ujasiriamali katika sekta ya madini, hususan wenye taaluma za sayansi, uhandisi, mazingira, uhasibu, mawasiliano na uendeshaji wa mitambo.

Maonesho ya 12 ya Biashara ya Kimataifa Zanzibar yataendelea hadi tarehe 16 Januari, 2026, ambapo wananchi wote wanakaribishwa kutembelea banda la Tume ya Madini ili kupata elimu, machapisho ya taarifa na kubaini fursa mbalimbali za uwekezaji na kushiriki katika sekta ya madini inayokua kwa kasi nchini Tanzania.





No comments:

Post a Comment