
Na Mwandishi Wetu - Dodoma
Watumishi wa Wizara ya Madini wamepatiwa mafunzo maalum ya Zimamoto, Uokoaji na Usalama Mahali pa Kazi, yaliyoandaliwa kwa lengo la kuongeza uelewa na utayari wa kukabiliana na majanga mbalimbali, hususan ajali za moto.
Mafunzo hayo yametolewa leo, Januari 27, 2026, na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania, yakihusisha zaidi ya washiriki 100 wakiwemo watumishi wa Wizara ya Madini pamoja na watoa huduma wa ulinzi na usafi.
Akitoa mada ya kinga na udhibiti wa majanga ya moto, Mratibu Msaidizi wa Mafunzo kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania, Steven Kante, amesema kuwa majanga mengi ya moto yanaweza kuepukika endapo kutakuwa na utayari wa kutosha, umakini, pamoja na uelewa sahihi wa matumizi ya vifaa vya kuzimia moto na utekelezaji wa hatua za kinga kabla na wakati wa dharura.
Aidha, amewataka watumishi hao kuhakikisha maeneo ya kazi yana vifaa vya kuzimia moto vilivyofanyiwa ukaguzi wa mara kwa mara, pamoja na kufahamu mahali vilipo na namna sahihi ya kuvitumia.
Amesisitiza umuhimu wa kutoa taarifa mapema pindi dalili za hatari zinapojitokeza, akibainisha kuwa hatua za haraka na sahihi katika dakika za awali za tukio la moto husaidia kuokoa maisha, mali na kuzuia madhara makubwa zaidi.
Kwa upande wa usalama wa matumizi ya paa la kupandisha watu au mizigo (lift) katika majengo, Mhandisi Lucas Daniel amesema kuwa watumiaji wanapaswa kuhakikisha lift hazizidishi uzito uliobainishwa, kuingia na kutoka kwa utulivu bila kusukumana wala kuchezea milango. Ameeleza kuwa lift hazipaswi kutumika wakati wa moto au dharura nyingine, akisisitiza matumizi ya ngazi katika hali hizo.
Awali, Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala wa Wizara ya Madini, Beatrice Matemu, amesema mafunzo hayo yameandaliwa mahsusi kwa watumishi wote wa Wizara pamoja na watoa huduma, ili kuhakikisha kila mmoja anakuwa na uelewa wa pamoja kuhusu masuala ya usalama na namna ya kukabiliana na majanga mahali pa kazi.
Amesisitiza kuwa Wizara ya Madini itaendelea kutoa mafunzo kama hayo mara kwa mara ili kulinda usalama wa watumishi na mali za Serikali, pamoja na kujenga utamaduni wa tahadhari, uwajibikaji na usalama kazini.
Kwa ujumla, mafunzo hayo yameonesha dhamira ya Wizara ya Madini katika kuimarisha usalama mahali pa kazi kwa kuwajengea watumishi uwezo wa kutambua, kuzuia na kukabiliana na majanga kwa ufanisi








No comments:
Post a Comment