BoT YAAGIZWA KUONGEZA UDHIBITI WA MIKOPO UMIZA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, January 27, 2026

BoT YAAGIZWA KUONGEZA UDHIBITI WA MIKOPO UMIZA



Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb) akiiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuendelea kuongeza udhibiti wa mikopo yenye riba kubwa (mikopo umiza) wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Mhe. Dkt. Neema Peter Majule, aliyetaka kufahamu Serikali imechukua hatua gani kwa watu ambao wamejinufaisha kwa mikopo yenye riba kubwa, bungeni jijini Dodoma.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha)


Na. Peter Haule, WF, Dodoma


Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb) ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuendelea kuongeza udhibiti wa mikopo yenye riba kubwa (mikopo umiza) ili wananchi wapate mikopo yenye tija.

Ametoa maagizo hayo bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Mhe. Dkt. Neema Peter Majule, aliyetaka kufahamu hatua zilizochukuliwa na Serikali kwa watu wanaojinufaisha kwa kutoza riba kubwa kwenye mikopo, hatua inayopunguza jitihada za Serikali za kuwakwamua wananchi kiuchumi hususani wanawake na vijana.

Mhe. Luswetula alisema kuwa Serikali imeanza kuchukua hatua kwa wote wanaokiuka taratibu zilizowekwa na Serikali za utoaji mikopo kwa kusitisha leseni zao na hatua nyingine za kisheria.

“Wizara ya Fedha imejipanga kuhakikisha taasisi zote zinazotoa mikopo zinafuata taratibu na tayari Serikali imeandaa rasimu ya kusimamia mikopo ya kidigitali inayotarajiwa kuanza kutekelezwa Mwaka wa Fedha 2026/2027”, alisema Mhe. Luswetula.

Akijibu swali la msingi kuhusu hatua zilizochukuliwa kudhibiti mikopo hatarishi inayotolewa na baadhi ya taasisi zisizo rasmi, Mhe. Luswetula alisema kuwa Serikali, BoT na wadau wengine, imechukua hatua mbalimbali za kudhibiti mikopo hatarishi yenye riba kubwa kwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi.

Alisema kuwa mikopo inapaswa kutolewa na watoa huduma wenye leseni kutoka BoT kwa mujibu wa Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya Mwaka, 2006 pamoja na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka, 2018.

Hatua nyingine iliyochukuliwa ni pamoja na kuwatambua na kuchukua hatua za kiutawala dhidi ya watoa mikopo wasioidhinishwa ambapo programu 69 za mikopo ya kidigitali zilizobainika kutoa mikopo bila leseni zilisitishwa na programu 126 zilifungiwa.

Vilevile kutoa Mwongozo maalum kwa watoa huduma za mikopo ya kidigitali ili kuhakikisha uwazi, uendeshaji wa kimaadili, utoaji wa taarifa kamili kuhusu gharama za mikopo pamoja na ulinzi wa watumiaji wa huduma za kifedha.

Mhe. Luswetula alilitaja eneo lingine kuwa ni pamoja na kuandaa rasimu ya kanuni za kusimamia mikopo ya kidigitali, ambazo zinatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2026/27 ambapo Kanuni hizo zinalenga kuimarisha udhibiti wa wakopeshaji wa kidijitali nchini Tanzania.

Aidha, Mhe. Luswetula alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha, imekuja na programu ya elimu ya fedha ya mwaka 2020/2021 hadi 2025/2026 ikiwa ni mpango maalum wa kutoa elimu kwa wananchi kwa makundi yote ambayo inalenga kuwawezesha wananchi kupata uelewa, maarifa na kuwajengea maarifa ya kusimamia mapato na matumizi na kufanya maamuzi sahihi katika kutumia huduma rasmi za kifedha.

Alisema kuwa Wizara ya Fedha kila mwaka imekuwa ikiadhimisha Wiki ya Huduma ya Fedha Kitaifa kuanzia mwaka 2021 na mwaka huu yamefanyika Jijini Tanga kuanzia Januari 21, lengo likiwa wananchi kupata elimu ya fedha.

Mhe. Luswetula alisema miongoni mwa Mikoa ambayo maadhimisho hayo yamefanyika kuanzia mwaka 2021 ni pamoja na Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na sasa Tanga.


Hadi sasa takribani mikoa 16 imefikiwa na huduma ya elimu ya Fedha na zaidi ya wananchi 64,000 wamefikiwa ikiwa ni pamoja na wanawake 40,000 na wanaume 24,000 na Halmashauri 94.

No comments:

Post a Comment