
Na Okuly Julius, OKULY BLOG – DODOMA
Matumizi ya teknolojia ya Akili Unde (Artificial Intelligence – AI) yanazidi kuwa muhimu katika kuboresha utendaji wa taasisi za umma, kuongeza ufanisi wa kazi na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi, hatua inayochochea Serikali kuwekeza katika kuwajengea uwezo watumishi wake kukabiliana na mabadiliko ya kidijitali.
Katika kuunga mkono juhudi hizo, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), wameandaa mafunzo maalumu ya siku tatu kwa Maafisa Waandamizi wa Serikali yanayolenga kuongeza uelewa na ujuzi wa matumizi sahihi ya teknolojia hiyo.
Mafunzo hayo yanayofanyika jijini Dodoma kuanzia Novemba 23 hadi 25, 2026, yanawakutanisha maafisa kutoka taasisi mbalimbali za Serikali kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutumia Akili Unde katika kurahisisha majukumu ya kiutendaji, uchambuzi wa taarifa na kufanya maamuzi yenye tija.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo Novemba 23,2026 jijini Dodoma, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Khatib Kazungu, alisema matumizi ya teknolojia mpya ni sehemu muhimu ya mabadiliko yanayoendelea duniani, hivyo ni muhimu kwa viongozi na watumishi wa umma kuwa na uelewa na uwezo wa kuitumia teknolojia hiyo katika kutekeleza majukumu yao.
Amesema Akili Unde ina nafasi kubwa katika kurahisisha shughuli za Serikali, kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu na kuboresha ubora wa maamuzi kupitia uchambuzi wa takwimu na taarifa mbalimbali.
Hata hivyo, Kazungu amesisitiza kuwa matumizi ya teknolojia hiyo yanapaswa kuzingatia misingi ya maadili, uadilifu na usalama wa taarifa, ili kuhakikisha mifumo ya kidijitali inatumika kwa uwajibikaji na kwa manufaa ya umma.
Ameeleza kuwa Dodoma, ikiwa ni makao makuu ya nchi na kitovu cha shughuli za Serikali, ina wajibu wa kuonesha mfano katika kupokea na kutumia ubunifu wa kiteknolojia unaoweza kuleta mageuzi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Lughano Kusiluka, amesema maendeleo ya jamii na kuendelea kuishi kwa mafanikio katika dunia ya sasa kunategemea kwa kiasi kikubwa matumizi sahihi ya teknolojia pamoja na uwezo wa kuibadilisha na kuitumia kulingana na mahitaji ya jamii.
Amesema Serikali imekuwa ikisisitiza umuhimu wa elimu na matumizi ya teknolojia kwa muda mrefu, hali iliyowezesha kuonekana kwa mabadiliko chanya na kuongeza ufanisi katika shughuli mbalimbali.
Aidha, Profesa Kusiluka amebainisha kuwa kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia inahitaji jamii na taasisi kujiandaa na kuendana nayo ili kunufaika na fursa zinazotokana na maendeleo hayo, akieleza kuwa mifumo na programu mbalimbali zimeendelea kurahisisha utendaji wa kazi na kuboresha utoaji wa huduma.
Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya vyuo vikuu, Serikali na wadau mbalimbali ni muhimu katika kuhakikisha teknolojia inatumika ipasavyo kukuza uchumi na kuleta maendeleo endelevu kwa jamii.
Akizungumzia namna mafunzo hayo yatakavyosaidia katika utekelezaji wa majukumu ya ukaguzi wa ndani, Tiba Ismail Baruti, Kaimu Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba, amesema teknolojia ya Akili Unde itakuwa nyenzo muhimu kwa wakaguzi katika kufanya uchambuzi wa taarifa, kulinganisha takwimu na kuandaa ripoti za kiutendaji.
Amesema matumizi ya teknolojia hiyo yatawasaidia wakaguzi kurahisisha maandalizi ya ripoti zinazowasilishwa kwa wakurugenzi na menejimenti, pamoja na kubaini mifumo na changamoto mbalimbali zinazohitaji maboresho katika halmashauri.
Naye Salum Mauga, mtumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, maarufu kama Mr. AI, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo watumishi wa umma walio chini ya TAMISEMI na taasisi zake ili kutumia teknolojia hiyo kuboresha utendaji wa Serikali na huduma zinazotolewa kwa wananchi kuanzia ngazi ya halmashauri.
Amesema Akili Unde ina uwezo wa kuchambua taarifa za miaka 10 hadi 20 kwa muda mfupi, jambo linaloweza kusaidia kubaini mwenendo wa mapato, changamoto za kiutendaji na maeneo yanayohitaji maboresho.
Mauga ameongeza kuwa teknolojia hiyo inaweza pia kutumika kusaidia utoaji wa taarifa kwa wananchi na kuwawezesha viongozi kufanya maamuzi yanayotegemea ushahidi wa takwimu badala ya kutegemea uzoefu pekee.
Amesisitiza umuhimu wa watumishi wa umma kuikumbatia teknolojia hiyo na kuitumia kwa ubunifu na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yao, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha matumizi ya teknolojia katika kuleta maendeleo ya nchi.
Mafunzo hayo yanajumuisha mada za kinadharia na vitendo zinazohusu matumizi ya Akili Unde katika mipango, uongozi, uchambuzi wa takwimu na utoaji wa huduma kwa umma.
Kupitia mafunzo hayo, washiriki wanatarajiwa kuongeza ujuzi wa kutumia teknolojia hiyo kwa ufanisi na uwajibikaji, hatua inayolenga kuimarisha utendaji wa taasisi za Serikali, kuongeza tija na kuboresha huduma kwa wananchi.


No comments:
Post a Comment