WABUNGE WAKOSHWA NA UTENDAJI KAZI WA WIZARA YA MALISILI NA UTALII - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, January 22, 2026

WABUNGE WAKOSHWA NA UTENDAJI KAZI WA WIZARA YA MALISILI NA UTALII


Na. Saidi Lufune, Dodoma


Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kupanua wigo wa shughuli za Utalii kwa kuviendeleza vivutio vya mbalimbali na kubuni mazao mapya ya utalii katika maeneo ya hifadhi.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Thimotheo Mnzava (Mb), Jijini Dodoma wakati kamati hiyo ikipewa mafunzo kuhusu majukumu ya Taasisi za Wizara. 

Mhe. Mnzava ameupongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Mamlaka ya Usimamizi ya Wanayamapori Tanzania (TAWA) kwa kujikita katika sekta ya uatalii jambo lililosaidia ongezeko la chaguo la vivutio vya Utalii na mapato ya Serikali. 

Aidha, ameitaka Wizara kuendelea kuzisimamia Taasisi zake ili kuendeleza sekta ya Utalii sambamba na kuboresha miundombinu mbalimbali ili kuweza kufikia azma ya Serikali ya kufikisha Watalii Milioni 8 ifikapo 2030. 

Baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo waliopata fursa ya kutoa ushauri wamezitaka Taasisi zilizopo chini ya Wizara, kuendeleza mahusiano mazuri baina yao na wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi sambamba na kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili ili waweze kuwa sehemu ya kuzilinda hifadhi hizo kutokana na manufaa wanayopata. 

Akihitimisha katika siku ya nne ya uwasilishaji kuhusu muundo na majukumu ya Wizara kwa Kamati hiyo ya Bunge, Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ameishukuru Kamati hiyo kwa usimamizi thabiti wa uhifadhi na shughuli za wizara kwa ujumla. 

Ameongeza kuwa Wizara itaendelea kuunga mkono sera ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuongeza matumizi ya nishati mbadala ili kuwawezesha wananchi kuachana na matumizi ya kuni na Mkaa jambo litakalosaidia kuondokana na migogoro mingi inayosababishwa na uvamizi wa maeneo ya hifadhi za misitu kwa ajili ya kukata kuni na mkaa jambo linalosababisha uharibifu wa mazingira. 

Ameihakikishia Kamati kuwa wizara itatekeleza kikamilifu maoni, ushauri na maelekezo ya Kamati na kurejesha majawabu kwa wakati kwa niaba ya Bunge. 

Waziri Dkt. Kijaji hii leo amewasilisha taarifa za Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Taasisi ya utafiti wa Misitu Tanzania, Mfuko wa Misitu Tanzania na Chuo cha Misitu-Olmotonyi (FTI).

Vilevile, kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb.), amewapongeza wajumbe kwa michango yao na kuahidi kwenda kuyafanyia kazi maelekezo ya kamati huku akisisitiza taasisi zote za wizara hiyo, kufanyakazi kwa utu wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku licha ya kutambua jukumu muhimu la kulinda na kuhifadhi rasilimali za taifa kwa kizazi cha sasa na kijacho

Viongozi wengine waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na na Naibu Katibu Mkuu, Bw. Nkoba Mabula, viongozi wa menejimenti ya wizara, Wakuu wa Taasisi na vyuo vilivyopo chini ya wizara hiyo.

No comments:

Post a Comment