WANAFUNZI WA USAGARA WAPATIWA ELIMU YA FEDHA WIKI YA HUDUMA ZA FEDHA TANGA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, January 22, 2026

WANAFUNZI WA USAGARA WAPATIWA ELIMU YA FEDHA WIKI YA HUDUMA ZA FEDHA TANGA


Kaimu Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha Bi. Dionisia Mjema akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Usagara kuhusu elimu ya usimamizi wa fedha binafsi ikiwa ni maadhimisho ya tano, yenye kaulimbiu "Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi" yanayoendelea katika Viwanja vya Usagara, Jijini Tanga.

Afisa Usimamizi wa Fedha wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bi. Grace Muiyaza akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Usagara kuhusu elimu ya usimamizi wa fedha binafsi ikiwa ni maadhimisho ya tano, yenye kaulimbiu "Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi" yanayoendelea katika Viwanja vya Usagara, Jijini Tanga.

Baadhi ya watumishi kutoka Wizara ya Fedha wakitoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Usagara kuhusu elimu ya usimamizi wa fedha binafsi ikiwa ni maadhimisho ya tano, yenye kaulimbiu "Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi" yanayoendelea katika Viwanja vya Usagara, Jijini Tanga.

Baadhi ya wanafunzi kutoka Shule ya Usagara wakipatiwa elimu kuhusu usimamizi wa fedha binafsi na wataalam kutoka Wizara ya Fedha ikiwa ni maadhimisho ya tano, yenye kaulimbiu "Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi" yanayoendelea katika Viwanja vya Usagara, Jijini Tanga.


Baadhi ya wanafunzi kutoka Shule ya Usagara wakipatiwa elimu kuhusu usimamizi wa fedha binafsi na wataalam kutoka Wizara ya Fedha ikiwa ni maadhimisho ya tano, yenye kaulimbiu "Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi" yanayoendelea katika Viwanja vya Usagara, Jijini Tanga.

Mwenyekiti wa Serikali za Mtaa Mkoa wa Tanga, Elizabeth Shangwe akielezea namna alivyoelewa kuhusu madhara ya mikopo kausha damu wakati akipatiwa elimu ya fedha na wataalam kutoka Wizara ya Fedha katika maadhimisho ya tano, yenye kaulimbiu "Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi" yanayoendelea katika Viwanja vya Usagara, Jijini Tanga.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Tanga)


Na. Chedaiwe Msuya na Eva Ngowi



Wizara ya Fedha kupitia Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha imeendelea kutoa elimu ya fedha kwa makundi mbalimbali ya jamii mkoani Tanga, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yanayoendelea katika Viwanja vya Usagara, jijini Tanga, kwa lengo la kuwajengea wananchi uelewa wa masuala ya kifedha na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.

Akizungumza wakati wa utoaji wa elimu katika darasa la Elimu ya Fedha, Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bi. Grace Muiyaza, alisema mafunzo hayo yanawalenga watumishi wa umma, wafanyabiashara wadogo, vikundi vya wajasiriamali, wananchi wa kawaida pamoja na wanafunzi kuanzia ngazi ya shule ya msingi, sekondari hadi vyuoni.

“Tuko hapa tunatoa mafunzo kwa makundi yote ya jamii ya Tanga. Lengo letu ni kuwajengea uelewa wa masuala ya kifedha na kuwawezesha kushiriki vizuri katika shughuli za kiuchumi,” alisema Bi. Muiyaza.

Alieleza kuwa katika darasa la siku hiyo, walikutana na wanafunzi wa Shule ya Msingi Usagara na kuwapatia elimu ya usimamizi wa fedha binafsi, akisisitiza kuwa elimu hiyo ni muhimu kwa watoto kwa kuwa nao hupata fedha kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo kwa wazazi wao.

“Watoto nao wanapata fedha kwa matumizi yao ya kila siku, hivyo ni muhimu wafundishwe mapema namna ya kusimamia fedha ili waweze kufikia malengo yao ya muda mfupi na mrefu,” aliongeza.

Bi. Muiyaza alisema darasa hilo lilikuwa shirikishi na wanafunzi walionesha uelewa mzuri kuhusu masuala ya msingi ya usimamizi wa fedha, hususan umuhimu wa kuweka akiba.

Alibainisha kuwa baadhi ya wanafunzi hupatiwa fedha nyingi zaidi ya mahitaji yao ya shule, hali inayowapa fursa ya kuanza utamaduni wa kujiwekea akiba mapema.

Katika hatua nyingine, alitoa wito kwa wazazi na walezi kuwalea watoto wao katika misingi sahihi ya kifedha, ikiwemo kutumia mifumo salama ya kutunza akiba badala ya njia zisizo salama kama vibubu au kuhifadhi fedha chini ya vitanda.

“Bado tunakutana na changamoto kubwa ya watu kuweka fedha kwenye sehemu zisizo salama na rasmi. Tunawahamasisha wazazi na jamii kwa ujumla kutumia benki, vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha, huduma za fedha kwa njia ya simu na kampuni za uwekezaji,” alisema.

Kwa upande wake, mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Usagara, Salma Rajabu, alisema elimu aliyopata imemfungua macho kuhusu umuhimu wa kuweka akiba na kuhifadhi fedha sehemu salama.

“Hapo awali nilijua fedha zinawekwa kwenye kibubu au chini ya kitanda, lakini sasa nimejifunza kuwa ni salama zaidi kuweka benki au kwenye simu. Nitawaelimisha wazazi wangu na kuwaomba wanifungulie akaunti ya akiba,” alisema Salma.

Naye Hassan Mohamed, mwanafunzi wa darasa la sita katika shule hiyo, alisema somo hilo limemsaidia kuelewa umuhimu wa akiba kwa maisha ya baadaye na namna ya kuwashauri wazazi wao kutumia njia salama za kuhifadhi fedha.

Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yanaendelea mkoani Tanga, yakilenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma za fedha na kuimarisha ujumuishaji wa kifedha kwa makundi yote ya jamii.

No comments:

Post a Comment