WAZIRI MAKONDA AKUTANA NA RAIS WA FIFA GIANNI INFANTINO, WAJADILI MAENDELEO YA MPIRA WA MIGUU TANZANIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, January 20, 2026

WAZIRI MAKONDA AKUTANA NA RAIS WA FIFA GIANNI INFANTINO, WAJADILI MAENDELEO YA MPIRA WA MIGUU TANZANIA


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Paul Makonda amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Shirikisho la Kandanda Duniani (FIFA) Bw. Gianni Infantino katika ofisi za FIFA zilizopo Jijini Rabat, nchini Morocco.

Katika mazungumzo hayo Mheshimiwa Makonda amemshukuru Bw. Infantino kwa ushirikiano mkubwa anaoutoa kwa Tanzania katika maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu na amemhakikishia kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali anayoiongoza inaunga mkono jitihada hizo na ipo tayari kushirikiana na FIFA.

Mheshimiwa Makonda amemueleza Bw. Infantino kuwa Tanzania inazo fursa nyingi za kuchangia katika maendeleo ya mpira wa miguu vikiwemo vipaji vya vijana wengi, maeneo ya kujenga miundombinu ya michezo na utashi wa kisiasa, na kwamba FIFA inakaribishwa kushirikiana na Serikali katika uwekezaji huo. 

Aidha, Mheshimiwa Makonda amemkaribisha Tanzania Bw. Infantino na amemwambia Tanzania ipo tayari kuwa mwenyeji wa matukio mbalimbali ya FIFA ikiwemo mashindano mbalimbali, mikutano na ziara za viongozi na wataalamu.

Kwa upande wake Rais wa FIFA Gianni Infantino amemshukuru Mheshimiwa Makonda na ujumbe wake kwa kumtembelea na kuzungumza nae na amesema FIFA ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika programu zake za maendeleo ambazo zitasaidia kutengeneza fursa kwa vijana kunufaika na mchezo wa mpira wa miguu ikiwemo ujenzi wa miundombinu na uendelezaji wa vituo vya ufundi.

Infantino ameipongeza Tanzania kwa kazi kubwa iliyofanywa na inayoendelea kufanywa na Serikali ya ujenzi wa miundombinu ya michezo kuelekea AFCON 2027 na amesema FIFA inaunga mkono jitihada hizo.

Katika mazungumzo hayo Mheshimiwa Makonda ameongozana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Gerson Msigwa, Balozi wa Tanzania nchini Morocco Mheshimiwa Ali Mwadini, Rais wa Shirikisho la Kandanda Tanzania (TFF) Bw. Wallace Karia, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Michezo Bw. Boniface Tamba na Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa Bi. Neema Msitha.
I'm

No comments:

Post a Comment