Na Benny Mwaipaja, Dodoma
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amesema kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa sekta ya mawasiliano katika kukuza uchumi jumuishi wa nchi kupitia mageuzi makubwa ya uchumi wa kidigitali, ulipaji kodi na uboreshaji wa huduma za jamii.
Mhe. Balozi Omar amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Kampuni ya Simu ya Vodacom ikiongozwa na Mwenyekiti wake wa Bodi, Bw. David Tarimo, katika Ofisi za Hazina-Treasury Square, Jijini Dodoma.
Aliishauri sekta ya mawasiliano nchini itumie fursa ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 iliyozinduliwa hivi karibuni, kuchangia zaidi maendeleo ya nchi Kupitia matumizi ya teknolojia ambayo itachangia kuongeza ukwasi kwa makundi mbalimbali wakiwemo vijana.
Mhe. Balozi Omar aliahidi kuwa Serikali kwa uopande wake itaendelea kuboresha na kuweka mazingira bora ya uwekezaji ili kuchochea na kukuza mchango wa sekta ya mawasiliano nchini katika kuboresha maisha ya wananchi na kuwawezesha wawekezaji kupata faida.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa VODACOM, Bw. David Tarimo, aliishukuru Serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji biashara kwa wawekezaji hali iliyoifanya sekta ya mawasiliano kuchangia kodi ya zaidi ya shilingi trilioni 1.1 katika mwaka wa fedha 2024/2025, huku Vodacom ikichangia zaidi ya shilingi bilioni 621 hadi ilipofikia mwezi Machi, 2025.
Aidha, Bw. Tarimo alieleza kuwa tangu Kampuni yake izinduliwe imewekeza zaidi ya shilingi trilioni 4.5 kwa ajili ya Kujenga miundombinu ya mawasiliano na na mwaka jana 2025 imesaidia jamii zaidi ya shilingi bilioni 3.7 kwa kufadhili miradi mbalimbali ikiwemo sekta za afya, elimu, mazingira na kuwawezesha vijana kiuchumi.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), Kaimu Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bi. Dionisia Mjema, Afisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom Tanzania, Bw. Philip Besiimire, Mkurugenzi wa Masuala ya Nje wa Vodacom Tanzania, Bi. Zuweina Farah, na maafisa wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha na Vodacom.







No comments:
Post a Comment