Benki ya NMB imekabidhi misaada ya madawati 100, viti 100, na meza 100 kwa shule mbili za msingi na moja ya sekondari wilayani Malinyi, mkoani Morogoro, vyote vikiwa na thamani ya Sh. Mil. 21.6. Msaada huu ni sehemu ya Sh. Bil. 7.4 zilizotengwa na benki hiyo kwa ajili ya kusaidia miradi ya kijamii katika sekta za elimu, afya, na mazingira kwa mwaka 2026, ikiwa ni asilimia moja ya faida baada ya kodi ya mwaka wa fedha ulioishia Desemba 31, 2025.
Meneja wa NMB, Kanda ya Kati, Bi. Janeth Shango, ndiye aliyekabidhi misaada hiyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Mhe. Sebastian Waryuba, aliyeipokea kwa niaba ya walimu wakuu wa Shule za Msingi Madibila Chini, Salamiti, na Shule ya Sekondari Kilosa Mpepo, zote za Malinyi.
Akizungumza katika hafla iliyofanyika shule ya sekondari Kilosa Mpepo, Bi. Shango alisema kuwa Shule ya Madibila Chini imepewa madawati 50, idadi sawa na waliyopewa Shule ya Msingi Salamiti, huku Shule ya Sekondari ya Kilosa Mpepo ikisaidiwa viti 100 na meza 100 kwa ajili ya wanafunzi.
Msaada huu ni uthibitisho wa ushiriki wa Benki ya NMB katika maendeleo ya kijamii na kurejesha kwa jamii kutokana na faida walioipata. Na ni kupitia michango hii, Benki ya NMB imeweza kusaidia katika mabadiliko kwenye sekta ya elimu na pia kuifanya kuwa mshindi wa tuzo ya Benki Kinara wa Uwajibikaji kwa Jamii kutoka Jarida la Global Banking and Magazine la Marekani.
Kwa upande wake, DC Waryuba, aliishukuru na kuipongeza Benki ya NMB kwa msaada huu wenye thamani ya Sh. Mil. 21.6, huku akibainisha kuwa kwa hesabu za haraka, madawati, viti, na meza hizi zitasaidia kuwatoa sakafuni watoto takribani 500 wa shule hizi waliokuwa wakisoma chini.
DC Waryuba aliongeza kuwa tayari NMB imefungua njia katika kuboresha elimu wilayani Malinyi na kuwataka wadau zaidi kufuata nyayo za benki hiyo kwa kujitolea kusaidia, huku akiwasisitiza walimu na wanafunzi umuhimu wa kutunza misaada hii ili kuwatia moyo wafadhili hao.




No comments:
Post a Comment