WAZIRI MKUU ATOA SIKU TANO KNCU ILIPE DENI LA SH. MILIONI 400 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, February 20, 2026

WAZIRI MKUU ATOA SIKU TANO KNCU ILIPE DENI LA SH. MILIONI 400


WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amemuagiza Mrajisi wa Vyama vya Ushirika mkoa wa Kilimanjaro ahakikishe Chama cha Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro (KNCU) kinalipa kwa mkupuo mmoja sh. milioni 400 ambazo chama hicho kinadaiwa na wakulima.

Ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Februari 20, 2026) aliposimama kusalimia wananchi katika eneo la Chekereni ambapo mkazi wa eneo hilo, Bi. Glory Sam kutoka Chama cha Mwika Kinyamvuo AMCOS alieleza malalamiko yake mbele ya Waziri Mkuu akitaja kusikitishwa na KNCU kuuza kahawa yao msimu wa mwaka 2021/2022 lakini hadi sasa hawajalipwa.

“Tuliuza kahawa yetu kwa zaidi ya shilingi milioni 600 lakini mpaka sasa tumelipwa shilingi milioni 200 pekee. Kwa kipindi chote hicho tumekuwa tukidai milioni 400 bila mafanikio.”

Dkt. Mwigulu amemtaka Mrajis ahakikishe kuwa hadi kufikia tarehe 25 Februari, 2026 Bodi hiyo iwe imekaa kikao na iamue ni mali gani zinauzwa ili kuweza kuwalipa kwa mkupuo wakulima hao.

“Tafuta kimojawapo kiuzwe, shilingi milioni 400 ipatikane na hawa watu walipwe mara moja. Hatuwezi kukaa na jambo moja miaka yote, kama kuna chama hakiwezi kulipa watu mnakaa nacho cha nini? Wananchi wanaumia, tabia ya kuzoea shida, matatizo na machozi ya watu hatuwezi kuivumilia.”

“Jambo limekaa miaka mitano mnataka likae miaka mingapi, upuuzi huu sitaki kusikiliza mnalipa lini? Jumatano ijayo mkae mtoke na majibu, tafuteni mtakachouza muwalipe watu pesa zao,” amesisitiza.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amekagua mradi wa ujenzi wa hospitali ya Halmashauri ya Manispaa ya Moshi inayojengwa katika Kata ya Ng’ambo kwenye manispaa hiyo.

Mradi huo ambao hadi kukamilika kwake unatarajiwa kugharimu sh. bilioni 6.59, hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 55 ya katika majengo ya huduma za wagonjwa wa nje, huduma za mama na mtoto kwa miundombinu ya sakafu ya chini na ya kwanza.

No comments:

Post a Comment