Bilioni 44.14 Kubadilisha Taswira ya Umeme Handeni - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, February 13, 2026

Bilioni 44.14 Kubadilisha Taswira ya Umeme Handeni


Waziri wa Nishati Mhe. Deogratius Ndejembi amesema mradi wa kimkakati wa ujenzi wa kituo cha kupoza umeme katika eneo la Mkata wilayani Handeni utagharimu shilingi bilioni 44.14 mpaka kukamilika kwake na utaimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Wilaya ya Handeni.

Akizungumza Februari 13, 2026 wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi, Waziri wa Nishati Mhe. Ndejembi amesema fedha hizo pia zitatumika kujenga njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 45 kutoka kituo cha Mkata hadi kijiji cha Kwamsisi.


Alieleza kuwa kwa muda mrefu wakazi wa Handeni walikuwa wakipata umeme kutoka Tanga, hali iliyosababisha upotevu mkubwa wa umeme njiani kutokana na umbali mrefu pamoja na kupungua kwa nguvu ya umeme. Kupitia mradi huu, sasa umeme utatoka Chalinze ambako ni karibu zaidi na Handeni, jambo litakaloongeza uthabiti wa huduma hiyo na kupunguza changamoto za kukatika mara kwa mara.

Kwa mujibu wa Waziri Ndejembi, kukamilika kwa kituo hicho kutaimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika wilaya za Handeni na Kilindi, kuchochea shughuli za uchimbaji wa madini ya graphite, kuvutia wawekezaji wapya na kuongeza mapato ya Shirika la Umeme kupitia wateja wakubwa watakaojiunga baada ya mradi kukamilika. Aidha, ajira zipatazo 120 zinatarajiwa kunufaisha wananchi wa eneo hilo.

Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya TBEA kutoka China na utekelezaji wake ulianza Agosti 17, 2023 na unatarajiwa kukamilika Novemba 16, 2026.

Kwa upande wake, mkazi wa Kwamsisi, Rashid Hamza amesema awali ilikuwa vigumu kuendesha shughuli za kiuchumi kwa kutegemea umeme kutokana na kukatika mara kwa mara. Alisema matarajio yao ni kuona mradi huo ukikamilika kwa wakati ili kuwawezesha kuongeza uzalishaji na kipato kupitia matumizi ya nishati ya umeme.

Jiwe la msingi la mradi huo limewekwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mwigulu Nchemba kama dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha miundombinu ya nishati kwa maendeleo ya wananchi.

No comments:

Post a Comment