“TUNASOGEZA HUDUMA ZA KISHERIA KARIBU ZAIDI NA WANANCHI” - MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, February 13, 2026

“TUNASOGEZA HUDUMA ZA KISHERIA KARIBU ZAIDI NA WANANCHI” - MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kupata huduma za ushauri wa kisheria katika Kliniki ya Sheria bila malipo inayotarajiwa kufanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam, kuanzia tarehe 16 hadi 22 Februari, 2026.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ametoa rai hiyo tarehe 13 Februari, 2026 wakati akizungumza na Vyombo vya Habari kuhusiana na Uzinduzi wa Kamati ya Ushauri wa Kisheria ngazi ya Mkoa na Wilaya pamoja na Kliniki ya Sheria bila malipo kwa wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam, ambapo Mgeni Rasmi katika uzinduzi huo anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza kuwa, lengo la Kliniki hizo ni kusogeza huduma za kisheria karibu zaidi na Wananchi.

“Lengo kuu la Kliniki hizi ni kusogeza huduma mbalimbali za kisheria kwa wananchi, ili wananchi wawe na utajiri wa huduma za kisheria”.Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Aidha, Mhe. Johari amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake katika kulinda, utawala wa Sheria ambao ndiyo msingi wa maendeleo ya nchi.

“Napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mhe. Rais kwa Uongozi wake, na zaidi katika eneo la msaada wa kisheria kwa wananchi, na kufanya huduma hizi ziwe zinapatikana kwa urahisi kwa wananchi.” Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Akizungumzia kuhusu Kamati za Ushauri wa Kisheria, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa lengo la kuanzishwa kwa Kamati hizo ni kutoa Ushauri wa Kisheria kwa Wananchi, Watumishi wa Umma na Viongozi wa umma ili kutatua changamoto za kisheria zinazojitokeza katika ngazi ya Mikoa na Wilaya.

Vilevile, Mhe. Johari ameeleza kuwa uwepo wa Kamati za Ushauri wa Kisheria, kutasaidia kupunguza mashauri au migogoro dhidi ya Serikali, malalamiko ya Kisheria kutoka kwa wananchi, vitendo vya uonevu na vinavyovunja sheria na taratibu, pia kamati hizo zitakuwa zikitoa elimu ya Sheria kwa umma katika kushughulikia changamoto mbalimbali katika maeneo yao.

No comments:

Post a Comment