BMT YAWATAKA VIONGOZI WAPYA CHANETA KUWA WABUNIFU KUINUA NETIBOLI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, February 11, 2026

BMT YAWATAKA VIONGOZI WAPYA CHANETA KUWA WABUNIFU KUINUA NETIBOLI


Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limewataka viongozi wapya wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) kuwa wabunifu ili kukuza vipaji vya vijana na kurudisha heshima ya mchezo wa netiboli nchini.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa vya chama hicho yaliyofanyika leo Februari 11, 2026, katika ukumbi wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, Afisa Michezo wa BMT, Apansia Lema, amesema viongozi hao wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanainua kiwango cha mchezo huo kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Amesisitiza kuwa viongozi hao wanapaswa kuhakikisha wanahamasisha ushiriki wa wasichana katika netiboli, kuibua vipaji kutoka mikoani na kuandaa wachezaji bora watakaoiwakilisha vyema Tanzania katika mashindano ya kimataifa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa CHANETA, Stella Mwangomale, ameahidi kushirikiana kwa karibu na viongozi wenzake katika kuimarisha netiboli nchini, hususan kwa kuibua vipaji vipya kutoka shuleni na kuendeleza ushauri mzuri wa viongozi waliopita.

Naye aliyekuwa Mwenyekiti wa CHANETA, Dkt. Devotha Marwa, amewataka viongozi wapya kuendeleza mazuri yaliyofanyika hapo awali na kuhakikisha netiboli inaendelea kuwa chachu ya kulitangaza taifa katika medani za kimataifa.

No comments:

Post a Comment