Wakati mijadala ya hatima ya mazingira duniani ikiendelea katika majukwaa ya kimataifa kama COP30, mikoa inayokabiliwa na changamoto ya mvua chache, hususan Dodoma, haiwezi kusubiri teknolojia za gharama kubwa. Badala yake, ubunifu wa ndani unaotoa suluhisho la moja kwa moja mashambani unaendelea kuwa msaada mkubwa kwa wakulima.
Moja ya mbinu zinazowasaidia wakulima ni kilimo funika, kinachohusisha upandaji wa mazao ya jamii ya mikunde kama choroko na fiwi. Mazao haya hufunika ardhi, kusaidia kuhifadhi unyevunyevu wa udongo na kupunguza upotevu wa maji, hali inayowezesha mimea kustahimili vipindi virefu vya ukame.
Mbali na hilo, wakulima wamekuwa wakitumia mashimo maarufu kama chololo. Mashimo hayo huchimbwa kwa mfumo maalumu ambapo sehemu ya udongo wa juu huwekwa chini na wa chini huwekwa juu. Mvua inaponyesha, maji hukusanyika ndani ya mashimo hayo badala ya kusambaa ovyo, hivyo kufyonzwa polepole na kutumika kwa muda mrefu na mazao.
Katika maeneo yenye mwinuko, matuta funika yamekuwa kinga muhimu dhidi ya upotevu wa maji na rutuba ya udongo. Kwa kawaida, mvua kubwa husababisha maji na udongo kuondoka kwa kasi, lakini matuta hayo husaidia kuyahifadhi maji na kuzuia mmomonyoko wa udongo.
Matuta hayo hutengenezwa kwa mtindo unaofanana na kilimo cha viazi, ambapo udongo wa chini huletwa juu na wa juu kubaki chini ili kuhifadhi unyevunyevu.
Mtafiti na Meneja kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Tawila Hombolo, Emmanuel Chilagane, anasema japokuwa mbinu hizi zimewasaidia wakulima wengi kukabiliana na ukame na kuongeza mavuno, zinahitaji nguvu kazi na gharama, hasa kwa wakulima wenye mashamba makubwa.
“Kwa wakulima wadogo mbinu hizi zinaweza kufanyika kwa kutumia jembe la mkono, lakini kwa wakulima wakubwa hali huwa tofauti. Kuweka matuta au mashimo katika shamba la hekari moja au zaidi huchukua muda mrefu na gharama huwa kubwa. Kuna umuhimu wa kupatikana kwa mashine ndogo za bei nafuu zitakazosaidia kuchimba mashimo ya chololo na kutengeneza matuta funika kwa urahisi,” anasema Chilagane.
Kwa mujibu wake, upatikanaji wa teknolojia rafiki kwa wakulima utawezesha mbinu hizo kutekelezwa kwa upana zaidi na kuchangia juhudi za Taifa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Naye mtafiti wa masuala ya udongo kutoka wilaya ya Kongwa, Ashura Ally, anasema mwitikio wa wakulima bado ni mdogo, kwani waliopokea na kutekeleza mbinu hizo ni wachache.
“Tunawaalika wakulima kujifunza kupitia mashamba darasa pamoja na kutoa vipeperushi vya elimu. Lengo ni kuhakikisha mbinu hizi zinaeleweka na kutekelezwa kwa vitendo,” anasema Ashura.
Simulizi za wakulima wa Kongwa na Kijiji cha Chololo zinaendelea kuonyesha kuwa suluhisho la mabadiliko ya tabianchi linaweza kupatikana mashambani.
Kinachohitajika sasa ni uwekezaji katika teknolojia nafuu na rafiki kwa wakulima ili mbinu hizi ziweze kutumika kwa upana zaidi na kuleta matokeo chanya katika uzalishaji wa kilimo.





No comments:
Post a Comment