WASIOENDELEZA ARDHI KWA MIAKA 3 KUNYANG’ANYWA, SHERIA YA ARDHI KUTUMIKA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, February 13, 2026

WASIOENDELEZA ARDHI KWA MIAKA 3 KUNYANG’ANYWA, SHERIA YA ARDHI KUTUMIKA


Serikali imewaagiza wananchi wenye hati za ardhi kuendeleza maeneo yao kwa kujenga kwa mujibu wa matumizi yaliyokusudiwa, ikisisitiza kuwa kisheria, endapo mmiliki hataendeleza ardhi hiyo ndani ya kipindi cha miaka mitatu, Serikali ina mamlaka ya kufuta hati na kuirejesha ardhi hiyo Serikalini.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo, Februari 12, wakati wa kufunga Kliniki ya Ardhi iliyodumu kwa siku 14 jijini Dodoma.

Dkt. Akwilapo amesema Sheria ya Ardhi inamtaka mwenye hati kuendeleza eneo lake kwa kujenga matumizi yaliyokusudiwa, na siyo kujenga ukuta au kibanda cha mlinzi pekee, bali kuhakikisha eneo linatumika kama lilivyopangwa.

Katika kliniki hiyo ya ardhi, jumla ya wananchi 4,597 walihudumiwa, huku hati 1,598 pekee zikichukuliwa.
Waziri amewaomba wananchi kufika kuchukua hati zao zilizosalia, akibainisha kuwa kuna hati 2,370 ambazo bado zipo ofisini hazijachukuliwa.

Katika hatua nyingine, Dkt. Akwilapo ametangaza kuanzishwa kwa “Wiki ya Samia ya Ardhi” ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

 Amesema kuanzia Machi 2 hadi Machi 7, 2026, ofisi za ardhi nchini zitatoa huduma kwa wanawake pekee, kwa lengo la kuwawezesha na kuwasaidia kumiliki na kutatua changamoto za ardhi.

Amesema hatua hiyo inalenga kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuhakikisha wanapata haki zao za kumiliki ardhi kwa mujibu wa sheria.

No comments:

Post a Comment