
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu, amewataka Wakuu wa Vitengo vya Habari na Mawasiliano Serikalini kutumia kikamilifu majukwaa ya mitandao ya kijamii katika kutangaza na kuelimisha jamii kuhusu kazi mbalimbali zinazotekelezwa na Serikali, hususan katika eneo la kujenga kizazi chenye usawa kupitia haki za kiuchumi.
Dkt. Jingu ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati wa kikao kazi cha kujenga uelewa kuhusu Programu ya Kizazi Chenye Usawa, kilichowakutanisha Wakuu wa Vitengo vya Habari na Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali za Umma.
Amesema kuwa bila kuwepo kwa usawa katika jamii, haitawezekana kujenga kizazi chenye maendeleo ya kweli na endelevu, hivyo juhudi za Serikali katika kuhakikisha haki za kiuchumi kwa makundi yote zinapaswa kuwasilishwa ipasavyo kwa wananchi kupitia vyombo vya mawasiliano, hususan mitandao ya kijamii.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii ambaye pia ni Mratibu wa Programu ya Kizazi Chenye Usawa, John Mapunda, amesema kuwa lengo la kutoa mafunzo hayo kwa Wakuu wa Vitengo vya Habari na Mawasiliano Serikalini ni kuwawezesha kufikisha kwa ufanisi ujumbe kwa jamii kuhusu mafanikio, fursa na mabadiliko chanya yaliyopatikana kupitia utekelezaji wa programu hiyo.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini TAMISEMI, Roida Andusamile, amesisitiza umuhimu wa uratibu na mshikamano miongoni mwa vitengo vya mawasiliano serikalini ili kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa lugha inayoeleweka.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Raymond Mushumbusi, amesema baada ya kupatiwa uelewa kuhusu Programu ya Kizazi Chenye Usawa inayotekelezwa nchini, wao kama waratibu wa mawasiliano ya programu hiyo wameipokea na kuahidi kushirikiana na Wizara za Kisekta katika utekelezaji wake.





No comments:
Post a Comment