DKT. MWIGULU AIPA WIZARA YA MAJI WIKI MBILI. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, February 19, 2026

DKT. MWIGULU AIPA WIZARA YA MAJI WIKI MBILI.


Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba ameipa Wizara ya Maji kipindi cha wiki mbili kuhakikisha inakamilisha mchakato wa upatikanaji wa mkandarasi wa ujenzi wa mradi wa maji kutoka chanzo cha Ziwa Chala.

Ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Marangu-Kitowo, Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro baada ya kupokea taarifa za ujenzi wa Mradi wa Maji kutoka chanzo cha ziwa Chala, Ujenzi wa mradi wa barabara Holili(Rotima)-Tarakea(Nayemi), pamoja kuweka jiwe la msingi la Shule ya Sekondari Stephen Moshi Technical.

Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amesema kuwa ujenzi wa mradi huo unapaswa kuanza kutekelezwa kwani unategemewa kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika Wilaya nzima ya Rombo.

Kwa upande wake Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema kuwa Wizara haitakuwa kikwazo katika utekelezaji wa mradi huo na watahakikisha katika kipindi cha siku 14 wanampata mkandarasi wa mradi huo.

Mradi wa maji ziwa Chala unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 8.66 na utanufaisha wananchi 34,104 katika vijiji 14 vya wilaya ya Rombo.

Kadhalika Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amemuagiza Waziri wa Fedha kuhakikisha anatafuta fedha kwa ajili ya kufanya malipo ya awali kwa mkandarasi ili aanze ujenzi wa mradi wa barabara Holili(Rotima)-Tarakea(Nayemi) kilomita 52.8

Mradi huo ambao utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 28 unapita mpakani mwa Tanzania na Kenya na unategemewa kusaidia kukuza shughuli za kijamii, kiuchumi pamoja na utalii.

Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Shule ya Sekondari Stephen Moshi Technical ambayo itagharimu shilingi bilioni 1.6 Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amesema kuwa shule hiyo ni kielelezo cha uwepo wa kiongozi mwenye maono na mipango.

“Ndani ya muda mchache sana zimejengwa shule zaidi ya 103 za aina hii nchi nzima” Amesema Dkt. Mwigulu.

Mradi huo utahusisha Ujenzi wa madarasa 08, ofisi 02, chumba 01 cha TEHAMA, maabara ya kemia na baiolojia, mabweni 4 ya wasichana na wavulana, bwalo 01, karakana 01 ya magari, matundu 08 ya vyoo vya wasichana na wavulana na Kichomea taka.

Pia utahusisha uchimbaji wa kisima cha maji cha ardhini, jengo la utawala na nyumba 01 ya mtumishi.



No comments:

Post a Comment