DKT.JAFO HAKUNA KULALA: AENDELEZA KAMPENI YA “KILA MTU ATIBIWE KWAO” KISARAWE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, February 27, 2026

DKT.JAFO HAKUNA KULALA: AENDELEZA KAMPENI YA “KILA MTU ATIBIWE KWAO” KISARAWE



Mbunge wa Jimbo la Kisarawe,Mhe.Dkt. Selemani Jafo, ameendelea kuonesha dhamira yake ya dhati katika kuboresha huduma za afya kupitia kampeni yake ya “Kila Mtu Atibiwe Kwao”, inayolenga kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na zahanati ili kusogeza huduma karibu na wananchi.

Akiwa katika ziara ya kuwashukuru wananchi wa Kitongoji cha Kola, Jafo amechangia tofali 1,500 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati mpya itakayohudumia wakazi wa eneo hilo.

"Mchango huo ni sehemu ya mkakati mpana wa kupunguza adha ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu, hususan wajawazito, watoto na wazee ambao kwa muda mrefu wamekumbana na changamoto ya kukosa huduma za afya karibu na makazi yao."amesema Dkt.Jafo

Akizungumza na wananchi, Dkt.Jafo amesisitiza kuwa afya ni haki ya msingi kwa kila mwananchi na kwamba ni wajibu wa viongozi kuhakikisha huduma hizo zinapatikana kwa urahisi bila usumbufu.

Ameeleza kuwa kampeni ya “Kila Mtu Atibiwe Kwao” inalenga kukamilisha ujenzi wa zahanati katika kila kijiji ndani ya jimbo hilo, ili kuimarisha ustawi wa jamii na kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika.

Aidha amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2020 hadi 2025, aliweza kuhamasisha ujenzi wa zahanati 27 kupitia ushirikiano wa Mfuko wa Jimbo, Halmashauri, Serikali Kuu pamoja na wadau wa maendeleo.

Amesema mafanikio hayo yanatoa msingi imara wa kuendeleza juhudi zaidi katika awamu ijayo.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Masaki, Pili Kondo Chamgui, amempongeza Dkt.Jafo kwa juhudi zake za kuwajali wananchi. Ameeleza kuwa kwa sasa vijiji vyote vya kata hiyo vina zahanati, huku Kituo cha Afya cha Masaki kikiwa kinatoa pia huduma za upasuaji, hatua iliyopunguza kwa kiasi kikubwa rufaa zisizo za lazima.

Ameongeza kuwa ujenzi wa zahanati katika Kitongoji cha Kola utakuwa mkombozi mkubwa kwa wakazi wa eneo hilo ambao hulazimika kusafiri zaidi ya kilometa sita kufuata huduma za afya katika kijiji mama cha Kisanga.

Nao,Wananchi wa Kitongoji cha Kola, wameeleza shukrani zao kwa mbunge huyo, wakisema amesikia kilio chao cha muda mrefu cha ukosefu wa huduma za afya karibu na makazi yao. Walisema changamoto hiyo ilikuwa ikiweka maisha yao hatarini hasa wakati wa dharura za kiafya.

Kwa ujumla, kampeni ya “Kila Mtu Atibiwe Kwao” inaendelea kuleta matumaini mapya kwa wananchi wa Kisarawe, huku ushirikiano kati ya viongozi na jamii ukiwa chachu muhimu ya kusogeza huduma bora za afya karibu zaidi na wananchi.

No comments:

Post a Comment