
Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango (NPC), Dkt. Fred Msemwa,akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya maandalizi ya kuanza kwa utekelezaji wa Dira 2050, Februari 01, 2026 jijini Dodoma.
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango (NPC), Dkt. Fred Msemwa, amesema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unalenga kuhakikisha kila Mtanzania anastawi bila kujali hali yake, kwani dira hiyo imebeba matumaini ya wananchi na inasisitiza ustawi wa pamoja, mshikamano na ushiriki wa kila mmoja katika ujenzi wa Taifa.
Ameeleza kuwa Dira 2050 ni alama ya umoja wa kitaifa na ina dhamira thabiti ya kutomuacha nyuma Mtanzania hata mmoja.
Dkt. Msemwa ameyasema hayo Februari 01, 2026 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya maandalizi ya kuanza kwa utekelezaji wa Dira 2050, ambao utaanza rasmi Julai 1, 2026, akisisitiza kuwa ni muhimu kwa wananchi kufuatilia na kuelewa mipango iliyoundaliwa ili kutekeleza dira yao.
Amefafanua kuwa Dira 2050 ilizinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 17 Julai 2025, na Serikali ikaielekeza NPC kuandaa mipango ya utekelezaji wake, ikiwemo Mpango Elekezi wa Muda Mrefu wa Miaka 25 (2026/2027–2050/2051), Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2026/2027–2030/2031) na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027.
Dkt. Msemwa amesema mipango hiyo imepitia mashauriano ya kitaalamu na itawasilishwa Bungeni tarehe 2 Februari 2026 kwa ajili ya kujadiliwa na kuidhinishwa kabla ya kuanza kutekelezwa.
Aidha, NPC imezingatia uzoefu wa utekelezaji wa Dira ya 2025, imeandaa nyenzo mbalimbali za ufanisi, na iko katika hatua za mwisho za kukamilisha Mfumo wa Kielektroniki wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Miradi ya Taifa (NPMIS) utakaotumika kufuatilia utekelezaji wa Dira 2050 kuanzia Julai 2026, huku wananchi na wadau wakihimizwa kufuatilia kwa karibu mchakato huo bungeni kwani mipango hiyo ndiyo msingi wa mustakabali wa maendeleo ya Taifa.




No comments:
Post a Comment