
Na Asteria Muhozya
Tanzania ilishiriki kikamilifu kwenye Kongamano la Kimataifa la Mining Indaba lililofanyika Februari 8 -12, 2026 nchini Afrika Kusini huku ujumbe wake ukiongozwa na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde na kuwakilishwa na vyama mbalimbali vya wachimbaji, taasisi za fedha, kampuni za kisheria, wafanyabiashara, watoa huduma migodini na wanawake wenye shauku ya kubadilisha taswira ya Sekta ya Madini nchini.
Miongoni mwao aliibuka Leminatha Cornel Kabigumila, Mkurugenzi Mtendaji na mwanzilishi wa Kampuni ya RARE Mining East Africa Limited ambaye ametengeneza historia ya kipekee na amekuwa kielelezo kwamba wanawake wanaweza kushiriki na kufanya vizuri katika uchimbaji madini Tanzania na barani Afrika.
Ikiwa ni mara yake ya kwanza kushiriki kwenye kongamano la Mining Indaba, Leminatha alishinda tuzo ya Mwanamke Mjasiriamali Sekta ya Madini iliyotolewa na Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wanawake Afrika (AWIMA) kwenye Kongamano la Mining Indaba ikithibitisha mchango wake mkubwa katika Sekta ya Madini Afrika na Tanzania. Hii si tuzo ya kwanza kwa Leminatha, pia, amekwisha kupata tuzo tatu za mchimbaji bora, mlipaji bora wa kodi za Serikali, na mwanamke bora mchimbaji kupitia tuzo za *“Usiku wa Madini”* tukio la kila mwaka kupitia Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania ambao hutumika pia kama sehemu ya kutambua mchango wa kampuni na wachimbaji bora waliofanya vizuri katika Sekta ya Madini Tanzania.
Katika mahojiano maalum na Madini Diary, Leminatha anasema, “sikujua kama nitapata tuzo hii. Nilikwenda Indaba kupata maarifa na kushirikiana na wenzangu, lakini zaidi ya matarajio yangu, nilipata tuzo. Hii ni ishara kuwa juhudi za kweli hutambuliwa.”
Sekta ya Madini Inavyoweka Mazingira wezeshi kwa kila mwenye nia
Leminatha anasisitiza kuwa Sekta ya Madini Tanzania imeweka mazingira rafiki kwa kila mtu anayetamani kuingia, bila kuogopa changamoto za mila, desturi, nk, anatoa mfano wa Afisa Madini Mkazi Samweli Shoo, sasa anafanya kazi Mkoa wa Kimadini Geita aliyemwamini na kumsaidia kupata leseni yake ya kwanza, jambo lililofungua mlango wa biashara ya madini kwa uwazi na heshima.
“Afisa Shoo alikuwa wa kwanza kuniamini na kunipa leseni. Hii ilinipa nguvu ya kuthubutu zaidi, kuanzisha biashara ya madini, na kuendelea mbele bila hofu. Sekta hii inatupa nafasi ya kuanzisha na kuendeleza shughuli zetu kikamilifu," Ninaishukuru Wizara, Maafisa Madini wote na vyama vyote vya wachimbaji wanawake," anasema Leminatha.
Aidha, kampuni za sheria kama Breakthrough Attorneys, taasisi za fedha ikiwemo benki ya NMB zilizoshiriki kongamano la Mining Indaba ambazo zilisaidia kuwahakikishi wenye nia ya kuweza nchini uhakika wa mikopo na msaada wa kisheria au ushauri wa kitaalamu wanapowekeza nchini pamoja na kuitangaza Sekta ya Madini nje ya mipaka ya Tanzania ikidhibitisha uwezo wao kila anayetamani kuingia Sekta ya Madini nchini anaweza kusaidika.
Masomo Muhimu Kutokana na Tuzo na Safari ya Kazi
Leminatha anashirikisha masomo makuu aliyoyapata: uadilifu na uwazi - huduma zote zinatolewa bure, kwa uwazi, na bila rushwa, na malipo yote hupitia mfumo rasmi wa Serikali; uthubutu na kutokukata tamaa. Aidha, anasema mafanikio yanahitaji bidii, moyo thabiti, na kukabiliana na changamoto bila kuogopa. Anayataja mafunzo mengine kama kujifunza kila wakati; mikutano ya kimataifa inafungua milango ya maarifa mapya na mtazamo mpana juu ya Sekta ya Madini, ikiwasaidia wachimbaji kuongeza thamani ya rasilimali zao na ushindi wa mwanamke mmoja ni ushindi wa jamii nzima, na ni kielelezo cha jinsi wanawake wanavyoweza kubadilisha mtazamo wa sekta.
Pia, Leminatha amefupisha mtazamo wake wa kimataifa, akisema, ‘’ushiriki wangu kwenye Mining Indaba umenipa mtazamo mpana wa kimataifa juu ya Sekta ya Madini na thamani ya hazina zetu za Tanzania, tunaweza kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi,".
"Nimejifunza kuongeza thamani ya madini kwa ubunifu, uwajibikaji kwa jamii, na uendelevu wa uwekezaji, huku nikiona namna wanawake wanavyoshika nafasi muhimu katika majukwaa makubwa ya kimataifa. Hii imenitia moyo kuendelea kusimama imara na kutimiza malengo bila kuogopa changamoto," anasema Leminatha.
Leminatha anahimiza wanawake kuanza kidogo, kuthubutu, kutokukubali majibu ya hapana bila kujaribu na kusisitiza ushindi wa mwanamke mmoja ni ushindi wa jamii nzima. "Tuzo hii ni ishara kuwa tunatambuliwa, kwamba ndoto zetu zinawezekana, na kwamba hatupaswi kukata tamaa," anasema.
Kwa sasa, Leminatha Kabigumila si tu mwanamke mchimbaji mwenye mafanikio, bali ni kielelezo cha uwezekano wa wanawake katika Sekta ya Madini Tanzania na barani Afrika. Ushindi wake kwenye Mining Indaba, ni funzo la maisha, ishara ya uwezekano, na motisha kwa wanawake wote kuendeleza ndoto zao na kushirikiana kikamilifu katika Sekta ya Madini.
Leminatha kupitia kampuni yake ya RARE Mining, anamiliki leseni 21 za madini ya bati zinazofanya kazi katika eneo la Kyerwa Kagera na leseni za uchimbaji madini ya dhahabu Kahama, Shinyanga na Manyara huku akieleza, "nina leseni za dhahabu na dhahabu yangu naiuzia BoT, Dodoma,".
Kwa kuzingatia mafanikio yake na mazingira wezeshi ya sekta, hadithi ya Leminatha ni uthibitisho kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea kuweka sera na mifumo rafiki inayowawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchumi wa madini na kukua kwa mafanikio.



No comments:
Post a Comment