WAZIRI KOMBO AKUTANA NA BALOZI WA SINGAPORE NCHINI WAJADILI UMUHIMU WA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIDIPLOMASIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, February 27, 2026

WAZIRI KOMBO AKUTANA NA BALOZI WA SINGAPORE NCHINI WAJADILI UMUHIMU WA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIDIPLOMASIA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Singapore nchini Tanzania, Mhe. Douglas Foo kuhusu umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizi mbili.

Wakati wa mkutano huo uliofanyika Februari 26, 2026 katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam, Mhe. Waziri Kombo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alimkabidhi Balozi Foo ujumbe maalum kwenda kwa Rais wa Jamhuri ya Singapore, Mhe. Tharman Shanmugaratnam.

Katika mazungumzo yao, Waziri Kombo alieleza kufurahishwa na ziara ya Balozi Foo nchini na kwamba ziara hiyo imekuja wakati muafaka ambapo Tanzania inaendelea kutekeleza program zake mbalimbali za maendeleo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na nchi rafiki ikiwemo Singapore.

Aliongeza kusema, maeneo muhimu ya kuongeza ushirikiano baina ya Tanzania na Singapore ni pamoja na biashara na uwekezaji, kuhamasisha ushirikiano wa sekta binafsi, sekta ya uchukuzi, pamoja na kuimarisha ushirikiano katika maeneo kama teknolojia ya kidijitali na maendeleo ya miundombinu kama Bandari.

Kwa upande wake, Mhe. Balozi Foo aliipongeza Tanzania kwa kuendelea kudumisha utulivu wa kisiasa na kufanya mageuzi ya kiuchumi yanayoweka mazingira rafiki kwa uwekezaji. Alieleza utayari wa Serikali yake wa kuimarisha ushirikiano kupitia kubadilishana uzoefu, kujenga uwezo na kuendeleza ushirikiano wa taasisi mbalimbali.

Aidha, viongozi hao pia walibadilishana mawazo kuhusu masuala ya kikanda na kimataifa yenye maslahi ya pamoja na kuthibitisha dhamira yao ya kuendelea kushirikiana kupitia njia za kidiplomasia na ziara za ngazi za juu.

Mkutano kati ya Waziri Kombo na Balozi Foo ulihudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Felister Rugambwa pamoja na Maafisa kutoka Tanzania na Singapore.

Balozi Foo ambaye anaiwakilisha nchi yake kutokea Singapore yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku sita kuanzia tarehe 22 hadi 27 Februari, 2026 ambapo ameendelea kukutana na viongozi wa Serikali na Sekta Binafsi.

Ushirikiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na Singapore umetimiza miaka 46 tangu ulipoanzishwa rasmi mwaka 1980.






No comments:

Post a Comment